2014-12-09 12:12:39

Siku ya Haki Msingi za Binadamu Kimataifa!


Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Haki Msingi za Binadamu Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 10 Desemba anasema, wananchi wanapaswa kupaaza sauti zao dhidi ya viongozi wanaowanyima: watu au makundi ya watu haki zao msingi; mahali popote pale walipo bila kujali tabaka, maoni na maelekeo yao ya kijinsia.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, hii ni haki msingi kwa mtu binafsi inayoiwezesha jamii kuwa na utulivu na dunia kupata maendeleo. Umoja wa Mataifa unasimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, kwani pale watu wanapofurahia haki zao, mchakato wa maendeleo ya kiuchumi unazidi kupamba moto na jamii inaishi katika amani na utulivu.

Uvunjaji wa haki msingi za binadamu ni majanga yanayopaswa kudhibitiwa na Jumuiya ya Kimataifa, kwani yanaweza kusababisha maafa makubwa au uhalifu wa kivita. Kila mtu anawajibika kulinda na kutunza haki msingi za binadamu dhidi ya vitendo vya kutokuvumiliana au kwa kuwa na misimamo mikali.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anazitaka Serikali kuhakikisha kwamba, zinaheshimu na kuendeleza haki msingi za binadamu, kwa ajili ya mafao ya wengi. Umoja wa Mataifa unaendelea kusikiliza kwa makini kilio cha wale wanaodhulumiwa na kunyanyaswa, ili kulinda utu na heshima yao kama binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.