2014-12-09 08:41:59

Chuchumilieni Utakatifu wa maisha!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, amewataka waamini wa Jimbo Katoliki Kondoa, kuhakikisha kwamba, wanachuchumilia utakatifu wa maisha, kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo; Wakristo wawe ni chumvi na mwanga kwa Jamii ya Kondoa, kwa kuendeleza mchakato wa kuyatakatifuza mazingira, ili yaweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kardinali Pengo ameyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa anatabaruku Kanisa kuu la Roho Mtakatifu, Jimbo Katoliki Kondoa, ambalo hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko ameliweka kuwa chini ya Jimbo kuu la Dodoma, lakini kabla ya hapo, lilikuwa chini ya Jimbo kuu la Dar es Salaam. Tukio la kuliweka wakfu Kanisa, ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema anasema Kardinali Pengo kwenda kuyatakatifuza malimwengu.

Askofu mkuu Yuda Thadeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, akizungumza kwa niaba ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amewapongeza waamini wa Jimbo Katoliki Kondoa kwa kujifunga kibwebwe kukamilisha ujenzi wa Kanisa kuu la Roho Mtakatifu ambalo limetabarukiwa na Kardinali Polycarp Pengo. Amewataka waamini kuendelea kuitunza “Nyumba ya Mungu” ili iweze kuwa ni mahali pa kukutana na kuongea na Mwenyezi Mungu.

Kwa uapnde wake, Dr. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika Ibada ya kutabaruku Kanisa kuu la Roho Mtakatifu, Jimbo Katoliki Kondoa. Dr. Bilal amelipongeza Jimbo Katoliki la Kondoa kwa kujikita katika utoaji wa bora wa huduma kwa wananchi katika sekta ya elimu, afya, maji na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Amesema, kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Roho Mtakatifu Jimbo Katoliki Kondoa ni kielelezo cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu wake, kutokana na kazi yao njema. Ni ukweli usiopingika anasema Dr. Bilal kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma makini katika sekta ya afya, elimu na maendeleo ya watu, changamoto na mwaliko kwa Taasisi za Kidini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia watanzania kwa ari na moyo mkuu zaidi, sanjari na utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Utunzaji wa mazingira ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na wananchi wote kwa kushirikiana na wadau mbali mbali. Wilaya ya Kondoa, ilikuwa inasifika sana kwa utunzaji bora wa mazingira, lakini leo hii ni kati ya Wilaya ambazo zimekumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, unaotishia amani na usalama wa raia na mali zao. Kumbe, anasema Dr. Bilal kuna haja kwa wananchi wa Kondoa kujipanga upya ili kusimamia suala zima la utunzaji wa mazingira.

Dr. Bilal amelipongeza Jimbo Katoliki la Kondoa kwa kukanilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Itololo, kitakachotoa huduma ya upasuaji pamoja na kulaza wagonjwa, sanjari na kuanzisha huduma makini kwa mama na mtoto, ili kupunguza vifo na kuokoa maisha ya wanawake wajawazito na watoto wadogo kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015.

Mchakato wa Jimbo Katoliki Kondoa kuanzisha Sekondari mbili ni sehemu ya mwendelezo wa maboresho ya sekta ya elimu nchini Tanzania ili kuhakikisha kwamba, wanafunzi wengi zaidi wanapata fursa ya kujiendeleza zaidi, ili kupambana vyema na changamoto za maisha, jambo la msingi ni wanafunzi kuzingatia masomo, ili waweze kufanya vyema zaidi.

Dr. Bilal amewashukuru watanzania wote kwa sala na dua zao, wakati Bunge Maalum la Katiba lilipokuwa linaendelea na mchakato wa kupata Rasimu ya Katiba Mpya ya Tanzania, ambayo itapigiwa kura ya maoni, Mwezi Aprili 2015. Amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya maoni kama sehemu ya utekelezaji wa demorasia Kikatiba sanjari na kuendeleza: haki, amani na utulivu.

Watanzania wajenge moyo wa umoja, mapendo, uvumilivu na kuheshimiana kwani hii ni misingi mikuu inayojenga amani ya kweli, vinginevyo, Tanzania inaweza kujikita ikitumbukia katika migogoro na kinzani zisizo na msingi. Waamini wa dini mbali mbali nchini Tanzania wanapaswa kuheshimiana, kama kielelezo cha utekelezaji wa uhuru wa kuabudu pasi na shuruti.

Dr. Bilal amewataka wanzania wenye haki ya kupiga kura kujitokeza ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 14 Desemba 2014. Wananchi wawachague viongozi makini watakaowaletea maendeleo ya kweli.

Jaji mstaafu Damian Lubuva akizungumza kwa niaba ya waamini wa Jimbo Katoliki la Kondoa amewasihi waamini wenzake kuendelea kujisadaka kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Kanisa. Ujenzi wa Kanisa umekamilika, lakini bado wanawajibika kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo Jimboni Kondoa, kwa kujitoa kwa hali na mali bila ya kujibakiza hata kidogo.

Kanisa kuu la Roho Mtakatifu linahifadhi masalia ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Msimamizi wa Jimbo Katoliki la Kondoa. Ujenzi wa Kanisa hili ulizunduliwa kunako tarehe 7 Aprili 2002 na Askofu mstaafu Mathias Isuja Josefu. Kunako mwaka 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaanzisha Jimbo Katoliki la Kondoa na kumtea Askofu Bernadine Mfumbusa kuwa Askofu wake wa kwanza. Ibada ya kulitabaruku Kanisa imehudhuriwa na Watu wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Kondoa.

Habari zaidi kutoka Tabora zinasema kwamba, Askofu mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora wakati akirejea kutoka Kondoa kwenye Ibada ya kutabaruku Kanisa kuu la Roho Mtakatifu alipata ajali baada ya gari yake kugonjwa na Lori la mchanga hivyo kulazimika kupelekwa kwenye Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza, kwa matibabu zaidi. Padre mmoja alivunjika mkono na sista alipata majeraha makubwa, lakini Dereva na Padre mmoja walisalimika bila jeraha lolote, ingawa ajali yenyewe ilikuwa ni mbaya sana.

Habari hii imeandaliwa na Sara Pelaji, toka Idara ya habari Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Rodrick Minja, Radio Mwangaza, Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.