2014-12-09 08:41:05

"Baba Benedikto"!


Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika mahojiano maalum na Gazeti la "Frankfurter Allegemeine" linalochapishwa kila siku nchini Ujerumani anasema kwamba, wakati alipokuwa mwishoni mwa uongozi wake, alijisikia kuwa mchovu na mdhaifu kiasi kwamba, alihofia utekelezaji wa majukumu yake kikamilifu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kama angekuwa na nguvu kwa wakati ule, jambo moja tu ambalo angelitamani ni kuitwa "Vater Benedikt", "Baba Benedikto", kwake hili lilikuwa linamtosha wala hakutamani makuu!

Mahojiano haya ambayo yamepata mwangi katika vyombo mbali mbali vya habari ndani na nje ya Ujerumani, yanaonesha jinsi ambavyo kweli Baba Mtakatifu Mstaafu alivyokuwa amechoka na jambo hili analikiri kutoka katika undani wa moyo wake. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika mahojiano hayo, amegusia mambo mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa, lakini zaidi ni kukamilika kwa mapitio ya kitabu chake alichokuwa ameanza kukiandika kunako mwaka 1972, kinachojadili kuhusu udumifu wa Sakramenti ya Ndoa na uwezekano wa Kanisa kuwashirikisha katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, wanandoa waliooa au kuolewa na baadaye wakaachana na kuamua kuoa au kuolewa tena.

Alipoulizwa kwanini anaingilia na kuonesha msimamo wake katika mada ambazo zinaendelea kujadiliwa na Mababa wa Sinodi, Baba Mtakatifu mstaafu anasema kwamba, kitabu hiki kilikwishapitiwa hata kabla ya kuanza kwa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu iliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014, kumbe, haingilii wala hana mpango wa kuingilia majadiliano ya Mababa wa Sinodi kuhusu tema hizi ambazo bado ni tete katika maisha na utume wa Kanisa, wakati huu Kanisa linapojitahidi kutangaza Injili ya Familia.

Baba Mtakatifu mstaafu anasema, wanauhusiano mzuri sana na Papa Francisko, lakini anajitahidi kuwa mkiya, lakini waamini wanatambua kwamba, kwa sasa Papa Francisko ndiye Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwishoni Baba Mtakatifu mstaafu anasema kwamba, Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli yanakwenda sanjari na Nchi Takatifu, mahali ambapo Yesu Kristo, Mtu kweli na Mungu kweli alipozaliwa. Tukio hili ni muhimu sana kwa imani ya Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.