2014-12-08 09:12:58

Waamini wa dini mbali mbali duniani wana wajibu wa kujenga na kudumisha amani!


Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislam uliowajumuisha wasomi na wanazuoni kutoka sehemu mbali mbali za dunia, uliopania pamoja na mambo mengine kudumisha na kuimarisha majadiliano ya kidini na kitamaduni, ili kuweza kukabiliana kikamilifu na kinzani zinazojitokeza miongoni mwa waamini wa dini hizi mbili, umehitimishwa kwa wajumbe kutoa tamko la pamoja linawataka waamini wa dini hizi kufahamiana zaidi, ili kudumisha: haki, amani na utulivu.

Ujumbe wa Wakristo katika mkutano huu umeongozwa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na upande wa dini ya Kiislam, ujumbe wao uliongozwa na Mwana wa Mfalme El Hasan bin Talal kutoka Yordan. Kauli mbiu iliyokuwa inaongoza mkutano huu ilikuwa “Wakristo na Waislam waamini katika jamii”.

Waamini wa dini mbali mbali wanatambua changamoto ya vita na kinzani za kidini inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, hasa zaidi huko Mashariki ya kati, katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Dini kwa sasa inaonekana kuwa ni kichocheo cha vita na vurugu badala ya kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho kati ya watu. Wajumbe wameonesha furaha yao ya ndani kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewatia shime ya kuendelea kukutana mara kwa mara ili kufahamiana na hatimaye, kujenga umoja na udugu.

Kabla ya kuhitimisha mkutano huu, kulifanyika kikao cha hadhara ambacho kiliwashirikisha wanadiplomasia kutoka katika nchi na Mashirika mbali mbali ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican bila kuwasahau waandishi wa habari, waliofahamishwa mkakati kazi utakaotekelezwa na viongozi hawa kwa siku za usoni. Mkutano huu umeendeshwa katika mazingira ya kuheshimiana, kwa kusikilizana, ili kukuza na kudumisha upatanisho, haki na udugu, mambo msingi ambayo kwa sasa yanahitajika ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.