2014-12-08 08:52:16

Vatican inaendelea kukazia sera za ukweli, uwazi na uwajibikaji katika masuala ya fedha za Kanisa


Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uchumi katika mahojiano maalum na Gazeti la Herald anasema kwamba, hali ya fedha mjini Vatican ni nzuri kuliko ilivyokuwa inafikirika, kwani kuna kiasi kikubwa cha Euro kilichokuwa hakikuoneshwa kwenye Bajeti ya Vatican, lakini mchakato wa mabadiliko na muundo mpya wa fedha mjini Vatican unaokazia: ukweli, uwazi, kanuni na sheria za kimataifa kuhusu fedha unaanza kuonesha mafanikio makubwa.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, fedha ya Kanisa inatumika vizuri kwa ajili ya kusaidia mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kardinali Pell anasema, miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na usiri mkubwa kuhusu fedha hali ambayo ilikuwa ni hatari sana kwani ingeweza kulitumbukiza Kanisa katika kashfa ya utakatishaji wa fedha haramu.

Kashfa ya kuvuja kwa nyaraka za siri mjini Vatican ni mambo yaliyoacha uchungu mkubwa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Mchakato wa mabadiliko ulioanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican unaendelea kuonesha mafanikio makubwa kwa kuwa na udhibiti wa mali na fedha ya Kanisa, dhidi ya wajanja wachache wanaotaka kujitajirisha wenyewe.

Akizungumzia kuhusu taarifa hii, Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, fedha inayotajwa si fedha haramu, bali ni fedha ambayo haikuwa imeoneshwa kwenye bajeti ya Vatican na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha ushirikiano mkubwa zaidi wa taasisi mbali mbali katika udhibiti wa fedha ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, taarifa ya Bajeti ya Vatican iliyokuwa inapitishwa kila mwaka na Baraza la Makardinali kumi na watano, iligusa baadhi ya taasisi kubwa za Vatican na wala si vatican yote.

Padre Federico Lombardi pia anasema, kuna watu wawili waliokuwa wanafanya kazi kwenye Benki ya Vatican, IOR, wamefikishwa mahakamani kufuatia tuhuma za kujihusisha na kufanya manunuzi kinyume cha sheria kati ya mwaka 2001 hadi mwaka 2008 na kwamba, akaunti zao za Benki zimefungwa.
All the contents on this site are copyrighted ©.