2014-12-08 09:15:45

Ujambazi unatishia amani na usalama wa wananchi Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, CAR, katika ujumbe wake kwa waamini katika kipindi hiki cha Majilio wanasema kwamba, vitendo vya uhalifu, ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha ni mambo ambayo yanakwamisha mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu nchini humo. Kuna watu ambao wanatekwa nyara na watu wenye silaha hali ambayo inajenga hofu na wasi wasi kwa wananchi kuweza kutekeleza shughuli zao za kila siku kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao.

Kuna baadhi ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao, ili kutafuta usalama sehemu nyingine za nchi, hasa Bangui, Bambari na Batangafo. Kinzani zilizojitokeza kati ya waasi wa Seleka na Balaka zimepelekea mgawanyiko na mpasuko wa kitaifa, hali ambayo imetishia umoja na mfungamano wa kitaifa, kwa misingi ya udini. Hapa ikaonekana kwamba, kuna vita kati ya waamini wa dini ya Kiislam na dini ya Kikristo, jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote ule.

Lakini ikumbukwe kwamba, Waislam na Wakristo kwa miaka mingi wameishi kwa amani na utulivu; kwa upendo na mshikamano, huku watu wakisaidiana kwa hali na mali. Vurugu zenye mwelekeo wa kidini ni matokeo ya baadhi ya waamini kuwa na misimamo mikali ya kiimani, hali inayohatarisha uhuru wa kuabudu na matokeo yake ni kuvunjika kwa haki msingi za binadamu, kunakopelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Kikundi cha Seleka na Balaka, ili kusitisha vita, kinzani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia hayana budi kutekelezwa pamoja na kuhakikisha kwamba, Serikali inawashughulikia kikamilifu watu wanaojihusisha na magenge ya kihalifu, ili utawala wa sheria uweze kuchukua mkondo wake, ili watu waishi kwa amani na utulivu.

Maaskofu wanakumbusha kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu. Amani inaweza kulindwa na kudumishwa kwa misingi ya majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi, mafao ya wengi na haki msingi za binadamu.
All the contents on this site are copyrighted ©.