2014-12-08 10:19:54

Papa asema , Noel bila mwanga, si Noel.


Baba Mtakatifu Francisko , Jumapili jioni, alipeleka salaam na ujumbe wake wa matashi mema, kwa wakazi wa mji wa Gubbio , Kaskazini mwa Italia, ambako kila mwaka, sasa kumekuwa na utamaduni maalum wa kuwasha taa za mti Noel, Mti ulio mkubwa, kuliko miti yote ya Noel Dunia. Mti wa Noel ishara maalum ya kipindi cha Noel, kipindi cha kuzaliwa kwa mkombozi wa dunia.

Katika ujumbe huo, Papa amesema, wakati wa kuwasha taa za pango la Noel, tunacholenga zaidi ni kusema kwamba mwanga wa Kristo umo ndani yetu. Papa amesisitiza , Noel bila mwanga si Noel. Kwa jinsi tunavyowasha taa katika mti wa Noel , naiwe hivyo pia kuwasha mwanga katika roho zetu , katika mioyo yetu , ili kuonyesha ishara ya kusamehe wengine; na kwamba hakuna uadui unaotia tena giza la chuki na fitina moyoni. Kwamba kuna mwanga wa Yesu ndani ya moyo, ambao ni upendo na kusamehe. Papa ameomba ili kwamba hamu hii iwe kwa wote, kwamba, hiki ni kipindi cha kuwasha upya mwanga wa Kristo, mahali penye Pango.

Papa Francisko , amewashukuru wote kwa zawadi yao ya kujitolea kufanikisha tukio hili, ishara ya upendo wa Kristo aliyejitolea pia kwa ajili ya wokovu wetu. Kwao wote amewatakia heri, amani na furaha za dhati , ili kwamba, giza lisitawale tena nafsi , bali iwe sala na maombi kwa Bwana wa Msamaha. Huu ni wakati wa Noel, nafasi kubwa ya kufanya safi roho, na hakuna sababu ya kuwa na hofu, kumwendea Kuhani, mwenye huruma, mwenye kusamehe yote katika jina la Mungu, kwa sababu Mungu husamehe kila kitu.

Papa ametolea ombi lake ili kwamba, Mwanga huu uwe katika nyoyo za wote, katika familia zote, na katika mji huo wa Gubbio. Kwa imani huo Papa kwa kutumia teknolojia ya Tablet, tokea Makazi ya jengo la Mtakatifu Marta, la ndani ya Vatican, aliwasha taa za Mti wa Noel wa Gubbio, na kutoa Baraka za Kipapa kwa kumwomba Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, akisema Heri za Noel kwenu nyote, na pia mkumbuke kuomba kwa ajili yangu.
Sherehe ya mwaka huu ya kuwasha taa za mti huu wa Noel wa Gubbio, ziliandaliwa katika uwanja wa Wafia dini wa Gubbio na kuuunganishwa katika mtandao wa video wa Kituo cha Televisheni cha Vatican , ili kuliwezesha watu kufuatilia sherehe hizi , kumwona Papa akiwasha taa za mti wa Noel wa Gubbio tokea Vatican.

Sherehe ya Mti Noel wa Gubbio, zilianzishwa tangu mwaka 1981, tangu hapo hufanyika kila mwaka katika mji huo , kwa kufanikishwa na kundi la kujitolea la watu wanaoishi katika mteremko wa mlima Ingino, unaoelekea mji wa Gubbio, Mkoani Umbria. Tangu mwaka 1991, uliingia kitabu cha kumbukumbu cha utendaji usiokuwa wa kawaida Guinness Records. Papa Benedict XVI pia aliwasha taa za mti wa Gubbio mwaka 2011 na Rais wa Jamhuri ya Italia Giorgio Napolitano, aliwasha taa katika mti huo mwaka 2012. Taa za mti huu huendelea kuwashwa hadi jioni ya Januari 6.

All the contents on this site are copyrighted ©.