2014-12-08 08:58:06

Majilio ni kipindi cha: huruma, upendo na mshikamano


Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, katika ujumbe wake kwa kipindi hiki cha Majilio, Mama Kanisa anapiojiandaa kuadhimisha Sherehe ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu, anasema, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ilikabiliwa na matatizo na changamoto nyingi kiasi hata cha kukimbilia uhamishoni, ili kulinda maisha ya Mtoto Yesu yaliyokuwa hatarini.

Leo hii kuna umati mkubwa wa wakimbizi wanaotaka kusalimisha maisha yao huko Sudan ya Kusini, DRC, Syria na Iraq. Familia Takatifu ilihitaji kupata chakula na kuna Wasamaria wema waliweza kuwasaidia. Wakimbizi na wahamiaji wanateseka kwa kukosa chakula, mahali pa kulala na hawana fursa za ajira; lakini hawana budi kupata njia itakayowawezesha kulisha watoto na familia zao.

Caritas imekuwa ni Msamaria mwema kwa kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kwa kuwapatia chakula na malazi pamoja na kuwajengea uwezo wa kuendelea kujisaidia na kuzisaidia familia zao. Caritas Internationalis imekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wanaoishi huko Beirut, Lebanon pamoja na kuwasaidia wanawake wajasiriamali kupata soko la bidhaa zao, licha ya kuendelea kuzisaidia familia sehemu mbali mbali za dunia kupata mahitaji yake msingi kwa kupambana na: baa la njaa, umaskini, ujinga na maradhi.

Caritas Internationalis inaendeleza kampeni ya kuhakikisha kwamba watu wanakuwa na uhakika wa kupata chakula, kwa kupambana kufa na kupona na baa la njaa ambalo bado linaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kampeni hii inaanza kuonesha cheche za mafanikio nchini Brazil, Thailand, Afrika Mashariki na Bara la Ulaya. Caritas Internationalis inakumbusha kwamba, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni familia ya kila mtu, jitahidi kusaidia familia mbali mbali kwa moyo wa upendo na ukarimu kama ambavyo ungefanya kwa Familia Takatifu, yapata miaka elfu mbili iliyopita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.