2014-12-06 14:56:01

Siri ya maungamo!


Kwa waamini wanaojongea kupokea Sakramenti ya Upatanisho, wanaonja huruma Mungu na kuondolewa dhambi zao sanjari na kupatanishwa na Kanisa ambalo limejeruhiwa kutokana na dhambi zinazotendwa na watoto wake, lakini kwa njia ya mapendo, mfano na sala linashughulikia kwa bidii wongofu wa watoto wake. Wongofu ni hatua ya kwanza kwa mwamini kuweza kumrudia tena Yesu, kwa kufanya toba na kutumiza malipizi ya dhambi. RealAudioMP3

Maaskofu na Mapadre ndio wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho na wenye uwezo wa kusamehe dhambi kwa njia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Padre anapoadhimisha Sakramenti ya Kitubio anatekeleza dhamana na huduma ya mchungaji mwema, anayetafuta Kondoo aliyepotea; huduma ya Msamaria mwema anayeponya majeraha; huduma ya Baba mwenye huruma anayemngoja Mwana mpotevu aweze kurejea tena nyumbani. Hii ni huduma ya hakimu mwenye haki, huruma na mapendo. Kimsingi, Padre ni chombo cha huruma na mapendo ya Mungu kwa wakosefu.

Kwa kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha na utume wa Kanisa, Idara ya Toba ya Kitume, hivi karibuni imeandaa kongamano ambalo limewashirikisha watu mbali mbali, ili kuchambua kwa pamoja umuhimu wa kulinda na kutunza siri ya maungano; ambayo kwa mtu anayebainika kwamba, ameivunja anatengwa na Kanisa, kadri ya Sheria za Kanisa. Hapa wanahusika hata wale wanaotumia njia za mawasiliano ya kisasa ili kusambaza siri za maungano.

Kardinali Mauro Piacenza, Mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume anasema kwamba, siri ya maungano inakwenda sambamba na Sakramenti ya Daraja Takatifu na kwamba, wahudumu wa Sakramenti hii, hawana sababu wala kuruhisiwa kutoa kwa mtu yoyote yule siri za maungamo; lengo ni kuhakikisha kwamba, Mama Kanisa anatunza kwa heshima na upendo mkuu mahusiano ya ndani kabisa kati ya Mwenyezi Mungu na mwamini anayetubu dhambi zake. Kanisa linapania kulinda heshima ya mwamini na haki zake msingi.

Monsinyo Krzysztof Nykiel, Afisa katika Idara ya Toba ya Kitume anasema, Mama Kanisa kwa wakati wote wa historia yake, ametoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya Sakramenti ya Upatanisho; mahali ambapo mwamini anapata fursa ya kukutana ana kwa ana na Padre kwa ajili ya maungamo; dhamana inayojikita katika kanuni maadili, sheria za Kanisa na ufafanuzi wa kitaalimungu, kama ilivyofafanuliwa kwa kina na mapana wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Laterano uliofanyika kunako mwaka 1215 kwa kuweka sheria na adhabu kwa Wakleri watakaovunja siri ya maungamo.

Monsinyo Nykiel anasema, siri ya maungamo inawafunga hata watu wale ambao kwa bahati mbaya wameweza kusikia maungano kati ya mwamini na Padre; kwani hapa kinachosisitiziwa ni mahusiano kati ya muungamaji na Mwenyezi Mungu. Maungamo hayana budi kufanyika kwa kusikiliza kwa siri na wala si kutangaza hadharani, ndiyo maana Mama Kanisa anakazia utakatifu wa siri ya maungamo ambayo haiwezi kutolewa hadharani hata kama itampasa Padre kuyamimina maisha yake.

Wawezeshaji wakati wa kongamano hili wamekazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa mawasiliano kati ya watu hasa wakati huu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo inawezesha mwanadamu kuwa na mwingiliano mkubwa , hali ambayo wakati mwingine inamfanya mtu kuwa ni tegemezi. Wajumbe wamefahamishwa pia kuhusu siri ya maungamo mintarafu mwelekeo wa kifalsafa na kitaalimungu, kwa kukazia ukweli dhidi ya uongo; mahusiano ya dhati kati ya Kanisa kama taasisi na ukuu wa Mungu.

Kardinali Mauro Piacenza amekumbusha kwamba, maungamo yanamsaidia mwamini kupunguza mzigo wa dhambi, kwa kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu unayojionesha kwa namna ya pekee katika moyo wa toba na unyenyekevu. Baada ya mwamini kuondolewa dhambi zake, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, hakumbuki tena dhambi zilizotendwa na mwamini, kwani zimesamehewa kutokana na ukuu wa Mungu.

Wawezeshaji wamekazia pia umuhimu wa kupokea Sakramenti ya Upatanisho pamoja na mwamini kuendelea kusindikizwa katika hija ya maisha yake ya kiroho, ili aweze kufundwa zaidi kutoka katika undani wake. Kuna mwelekeo mkubwa kwa sasa vijana kutaka kusikilizwa kwa makini zaidi; kwa kujenga na kudumisha mahusiano yanayojikita katika ukweli, huruma na katika maelekeo ya kuweza kujipatia wokovu.

Kardinali Mauro Piacenza anasema haki ni njia nyingine ambayo inaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anampenda mwanadamu na kumtakia mema. Mwenyezi Mungu anatumia haki ili kupenda na kwamba, haki ni chemchemi ya mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.