Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma anapenda kuwaalika waamini
na watu wote wenye mapenzi mema kuungana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho
ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, inayoadhimishwa na Mama Kanisa
kila mwaka ifikapo tarehe 8 Desemba.
Maadhimisho haya yatafunguliwa kwa Kikosi
cha zimamoto kuweka shada la maua katika Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya
Asili, iliyopo kwenye Uwanja wa Spagna, kama kumbu kumbu endelevu iliyofanywa na Kikosi
cha Zima moto tarehe 8 Desemba 1857. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja
wa Spagna majira ya saa 10: 00 jioni na kulakiwa na viongozi wa Kanisa na Serikali.
Kardinali Vallini anasema, kutakuwepo na umati mkubwa wa wagonjwa watakaosindikizwa
na Chama cha Kitaifa cha Kuwahudumia Wagonjwa, UNITALSI, ili kutoa heshima yao kwa
Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili pamoja na kusalimiana na Baba Mtakatifu Francisko
ambaye katika maisha na utume wake, anaendelea kuwapatia wagonjwa na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii kipaumbele cha kwanza. Kimsingi, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa
Dhambi ya Asili inapania kuwa ni siku ya sala, tafakari na mshikamano na maskini.