2014-12-06 16:16:42

Ogopa utata wa maisha ya binadamu!


Niliwahi kumsikia dada mmoja akimwita mdogo wake Imakulata kwa ufupisho: “Makulataaa! Unaitwa na mama!” Jina Makulata jinsi alivyolitumia dada huyu linatokana na neno la kilatini “makula” maana yake ni doa au uchafu. Kinyume chake ni Imakulata, maana yake kutokuwa na doa au uchafu wala takataka yoyote ile. RealAudioMP3

Leo kanisa katoliki popote duniani linasherehekea sikukuu ya Bikira Maria Imakulata, yaani Maria msafi mbele ya Mungu, asiye na dhambi kwani alikingwa tangu kuzaliwa kwake. Katika kanisa fundisho hilo la Maria kuwa Immakulata linaitwa Dogma. Dogma hiyo ilitangazwa rasmi tarehe nane Desemba mwaka 1854 na Baba Mtakatifu Pius wa tisa. Toka hapo katika nchi nyingi duniani, kanisa katoliki limemchagua Imakulata kuwa mlinzi wa Taifa lao.

Kadhalika katika Afrika, kuna nchi nyingi, kama vile Jamhuri ya Congo na Jamhuri ya Muungano ya Tanzania wamemchagua Maria Imakulata kuwa mlinzi wa Taifa. Kwa nchi ya Tanzania sikukuu hiyo imepangwa siku moja kabla ya sikukuu ya kupata uhuru wake wa kisiasa toka kwa wakoloni. Dogma ni lugha tata isiyoeleweka kirahisi na mtu wa kizazi cha leo. Lakini yabidi ieleweke kuwa Dogma yoyote ile ni tamko la kibinadamu siyo amri ya Mungu.

Tamko hilo linatafsiri ukweli wa Neno la Mungu lililo katika Biblia. Kwa vyovyote, lugha hii ya kibinadamu ambayo ni Dogma inategemea sana mabadiliko ya hali halisi ya maisha ya jamii. Kwa hiyo dogma ni tafsiri ya maisha mbayo inabidi irandane na ukweli wa maisha. Dogma ya Bikira Maria Imakulata mkingiwa dhambi ya asili imewekwa hivi kwamba iweze kuigusa jamii yetu ya leo. Kwa maana hiyo, yaonekana hali ya maisha na matendo ya Mama huyu Maria yanalingana na hali halisi ya mazingira yetu ya sasa.

Ukweli huo hauna upinzani, kwani Maria alikuwa mtu kama sisi, alizaliwa kama watu wengine huko Galilea, alipokuwa msichana akampenda kijana Yosefu, na akategemea kuolewa naye wakiwa na malengo ya kupata watoto na kuijenga familia yao kadiri ya mila na desturi za utamaduni wa waana wa Ibrahimu. Akiwa sawa kama watu wengine, mama huyu alipambana pia na makashkash ya maisha, na alishawishiwa, kwani hata mwanae Yesu alishawishiwa pia. Tofauti ya Maria na watu wengine ni hii kwamba Mungu aliona katika Maria utayari kamili uliomvuta amchague kumtumia katika mradi wake wa kuukomboa ulimwengu.

Hebu tuiangalie sikukuu yetu katika mwanga wa somo la kwanza la leo ili tuweze kuelewa na kufaidika na dogma ya Imakulata. Fasuli hii inahusu kuanguka kwa Adamu na Eva katika dhambi. Habari hii imeundwa kadiri ya mantiki ya kifilosofia na teolojia ya wakati huo, na ni lugha ngumu kueleweka kwa watu wa sasa. Ukweli uliojulikana enzi hizo hadi leo kuwa sisi binadamu tumeathirika na dhambi ya asili aliyoitenda Adamu na mke wake Eva.

Hapo haieleweki ni kwa hoja ipi adhabu hiyo tupewe sisi tusiohusika na kosa walilolitenda wazee hawa. Ukweli ni kwamba habari hiyo isichukuliwe kuwa kama simulizi la kihistoria ya maovu yalivyotendwa na Adamu na Eva.

Fasuli hii inataka kutoa fundisho la kiteolojia linalojibu kwa lugha ya kimistiki (myth) maovu na utata wa maisha anaokumbana nao binadamu. Hasahasa inalenga kujibu swali la kwa nini kuna uovu, uharibifu, na ukosekanaji wa haki hata mauaji hapa duniani. Ukweli ni kwamba binadamu mwenyewe yaani wewe na mimi ndiyo Adamu na Eva. Ni sisi ndiyo tulio kinyume na mwito aliotuitia Mungu wa jinsi njema ya kuishi hapa duniani. Kutokana na ukweli huo, hata dogma ya Imakulata inadai kuitazama kwa kina na kuielewa kwa namna mpya.

Tuangalie kinaganaga maelezo na ujumbe wa anguko la wazee wetu wa kwanza. Mungu aliumba ulimwengu kwa muda wa siku saba, namba inayoonesha ukamilifu. Halafu inarudiwa kusemwa mara nyingi kuwa, baada ya uumbaji akaona kila kitu alichokiumba kuwa ni chema. Maana yake kulikuwa na amani, ushirikiano, wema kati ya Mungu na binadamu. Binadamu aliishi vyema na kwa amani hata kati ya bwana na bibi. Kila mmoja alijisikia kuwa ni zawadi kwa mwingine.

Katika mazingira mazuri kama hayo anajipenyeza nyoka. Huyo anafika na kushawishi kuvunja mahusiano hayo mazuri. Anamshawishi binadamu kumpindua Mungu, ili abaki mwenyewe wa kupanga na kuamua mambo yake. Hadithi za nyoka na shetani zinatokana na marabi wa kiyahudi waliokuwa wameathirika na mithi za mila za Wapersia.

Hao ndiyo walioanza kumwona shetani katika umbo la nyoka kuwa kama mpinzani au kinyume cha Mungu. Nyoka au shetani anaoneshwa kuwa ni mwerevu, mwongo na mjanja sana. Ujanja au werevu ambao ni udanganyifu wa kutaka kurubuni hekima ya Mungu na mapato yake unaishia kujirubuni wenyewe na kuvunjisha mahusiano na Mungu na ya wengine.

Mungu anamwita Adamu na kumwuliza “Uko wapi”. Ni tofauti na kuuliza “Upo wapi” yenye maana ya pahala. Bali aliuliza “Uko wapi?” akimaanisha anajisikiaje, ana hali gani hasa baada ya kujitenga na Mungu.

Sikiliza majibu ya Adamu na linganisha na kitokeacho katika historia ya binadamu. “Niliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.” Kwa hiyo pato la kwanza la kukata mawasiliano na Mungu ni kuwa mtupu bila kitu, kisha unajionea aibu mwenyewe.

Angalia pia leo ulimwengu wa watu waliomwacha Mungu na kufuata vichwa vyao jinsi wanavyoishi. Yote yanatokana na kujiweka sisi kwanza badala ya kumweka Mungu kwanza. Adamu anapodadisiwa zaidi anajietea, “ni mwanamke uliyenipa”. Kwa hiyo pato jingine la kuvunja mawasiliano na Mungu ni kuvunja mahusiano na wenzako.

Binadamu anamlaumu mke wake, ambaye Mungu amemweka kando yake. Mbaya zaidi, kosa linamrudia Mungu mwenyewe, analaumiwa jinsi alivyomuumba vibaya. Amemtengeneza mwanamke mwenye roho mbaya. Mwanamke naye anapita mulemule alimopita bwana wake. Anamlaumu nyoka.

Kwa namna fulani hata Eva naye anamlaumu Mungu kwa kuumba mambo vibaya. Kwa hiyo wazee hawa wote wawili kwa pamoja wanamlaumu Mungu kwa kuuumba vibaya ulimwengu huu. Mungu amekosea sana kuweka ndani mwetu uhalisia wa wema na ubaya. Ametuumba watu wenye mipaka ndiyo maana hatupo tu wema moja kwa moja, bali kuna nguvu ya kugoma kufanya hata mambo yake Mungu mwenyewe. Kwa hiyo Mungu mwenyewe amejipalia mkaa kichwa na ametujengea kiburi.

Hata hivyo swali linalozidi kutukereketa linabaki: Je huyo nyoka atakuwa ndani yetu hadi lini, yaani, uovu huo hauwezi kushindwa? Jibu la swali hilo linapatikana katika sikukuu ya leo. Habari njema ya sikukuu ya leo, imeanza hapa unapoona wazi kabisa jinsi shetani anavyoshindwa. Unamwona nyoka huyo hafiki mbali, kwani “Njia ya mwongo ni fupi, au “ndege mjanja hunaswa kwenye tundu bovu”. Hapa unaona wazi kwamba baada ya kuhojiana na Eva, Mungu hapotezi muda wake kumhoji nyoka, kwa sababu nyoka au ujanja na wongo huo ni sehemu ya binadamu.

Basi ujanja na wongo huo unaambulia kupata hukumu kali pale nyoka anapoambiwa: “Umelaniwa wewe kuliko hayawani wote walioko mwituni”. Kulaaniwa maana yake kutokuwa na uzao yaani ni kufa na kufifia kabisa. Kisha anaambiwa tena “utatambaa ardhini na kula mavumbi siku zote za maisha yako.”

Kwenda kwa tumbo hakumaanishi kwamba kabla yake nyoka huyu alikuwa na miguu na alitembea la hasha, bali ni lugha ya picha, kwamba sasa nyoka atagaagaa ardhini kama askari aliyeshindwa na kujeruhiwa anavyojigalagaza ardhini mbele ya shujaa aliyemteka. Maana yake nyoka atashindwa na kugaagaa chini baada ya kukatwa kichwa.

Hii ndiyo maana nzuri ya sikukuu ya leo. Kwamba shetani atashindwa. Toka hapa kila mmoja wetu katika maisha yake, ya imani, ya uongozi, ya kisiasa nk anaweza kuanza kufanya fikara zake. Kwamba sisi kumbe ni akina Adamu na Eva na tumepagawa na nyoka mwerefu, mwongo, mjanja, mdanganyifu.

Tunaalikwa kumwangalia Maria jinsi alivyoishi maisha yake yote akiwa na umoja na amani na Mungu. Hata kama katika Maria kulikuwa na huyo nyoka mwerevu, mjanja na mwongo, aliyemjaribu kumwepusha na mawazo na fikra za Mungu, lakini shetani huyo hakufanikiwa kumrubuni na kumwangusha.

Maria alikuwa daima mwaminifu kwa Mungu. Mama huyu pekee ni alama ya ushindi wa Mungu dhidi ya uovu wa ulimwengu. Ndiyo maana anaitwa Bikira Maria Immakulata. Sisi sote tumeitwa kuwa Imakulata. Tusikubali kuitwa “Makulataaa!”

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.