2014-12-06 15:02:05

Mashuhuda wa imani!


Wakristo huko Mashariki ya Kati licha ya madhulumu na nyanyaso wanazokabiliana nazo, bado wanaendelea kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kuna baadhi ya watu wanataka kuona kwamba, Wakristo wanafutika kutoka huko Mashariki ya Kati, lakini hata katika magumu yote haya, bado kuna Wakristo wanaendelea kushuhudia imani yao.

Kuna maelfu ya watu ambao wana madonda makubwa katika maisha yao; wanawake wanaoendelea kuombeleza kutokana na kuondokewa na wapendwa wao; wazee ambao hawana msaada tena; wakimbizi na wahamiaji wanaohofia usalama wa maisha yao pamoja na mateso makali ya wananchi wengi huko Mashariki ya Kati. Lakini katika mahangaiko yote haya, Wakristo watambue kwamba, Kanisa linaendelea kushikamana nao, ili kuwaonjesha upendo na mshikamano wa dhati.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko uliowasilishwa kwa Wakristo wa Mosul, nchini Iraq na Kardinali Philippe Barbarin wa Jimbo kuu la Lione, Ufaransa ambaye Jumamosi tarehe 6 Desemba 2014, ametembelea eneo hili kuonesha mshikamano wa Kanisa. Nyanyaso na madhulumu haya ni matokeo ya misimamo mikali ya kiimani na ukabila unaosababisha mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia pamoja na kuwataka kukana imani yao, mambo ambayo yanakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu.

Vita imekuwa ni sababu ya majanga makubwa kwa watu pamoja na uharibifu wa nyumba za ibad na urithi wa kitamaduni. Viongozi wa kidini wanadhamana ya kimaadili ya kukemea na kulaani vitendo vyote vinavyodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawapongeza Wakristo kwa ushuhuda wao makini na kamwe wasikate tamaa na kwamba, anaendelea kuwaombea nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu, ili kuweza kupata suluhu ya mateso na mahangaiko haya, ili hatimaye watu waweze kurudi katika makazi yao.

Baba Mtakatifu anawahakikishia kwamba, katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, atawakumbuka katika sala na maombi yake, ili Bikira Maria aweze kuwalinda na kuwasimamia katika ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake.All the contents on this site are copyrighted ©.