Tume ya uchaguzi nchini Zambia imetangaza kwamba, wananchi wa Zambia watafanya uchaguzi
mdogo hapo tarehe 20 Januari 2015 kufuatia kifo cha Rais Michael Chilufya Satta, kilichotokea
hivi karibuni nchini Uingereza. Kinzani na mipasuko ya kisiasa inayoendelea kujionesha
katika vyama vya kisiasa nchini Zambia haitazuia uchaguzi mdogo kufanyika kama ilivyopangwa.
Kutokana na changamoto hizi ambazo zinatishia usalama, amani na utulivu wa
wananchi wa Zambia, Jukwaa la Wakristo nchini Zambia limeunda Kikosi kazi "CCMG" kitakachosimamia
mchakato wa uchaguzi mkuu na hasa katika zoezi la kuhesabu kura, ambalo mara nyingi
limekuwa ni chanzo cha vurugu na kutoweka kwa amani. Lengo ni kutaka kudumisha misingi
ya haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, ili kweli mchakato wa demokrasia
uweze kushika mkondo wake na hatimaye, kuwapatia wananchi wa Zambia kiongozi atakayewaongoza
ili kujiletea maendeleo endelevu.
Kikosi kazi katika waraka wake kwa wananchi
wa Zambia kinasema, kinapenda kukazia na kudumisha misingi ya ukweli, uwazi na uhuru
katika mchakato mzima wa uchaguzi mdogo nchini Zambia. Ili zoezi hili liweze kufanikiwa
kuna haja kwa vyama vya kisiasa nchini Zambia kuchagua kiongozi bora atakayepimana
nguvu na wengine, ili hatimaye, Zambia iweze kumpata Rais mpya.
Wananchi wote
hawana budi kupania kujenga na kudumisha amani na utulivu wakati wote wa kampeni,
lakini zaidi siku ya kupiga kura, ili kutoa nafasi kwa wananchi kutumia haki yao ya
kikatiba kuchagua kiongozi anayewafaa. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba, inaunda
mazingira yatakayowezesha uchaguzi kuwa huru na wa kweli sanjari na kudhibiti rasilimali
fedha na watu, ili yote haya yatumike kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wananchi
wote wa Zambia. Waandishi wa habari watekeleze dhamana na utume wao kwa kuzingatia
kanuni maadili, weledi na sheria za nchi. Wanasiasa waepuke kampeni zinazojenga chuki,
uhasama na ukabila kati ya watu.
Vijana wasikubali kutumiwa na wanasiasa uchwara
ili kuvuruga amani na utulivu nchini Zambia, bali wahakikishe kwamba, viongozi watakaowachagua
ni wale wanaopania kuwapatia fursa za ajira pamoja na kudumisha amani na utulivu nchini
Zambia. Viongozi wa kijadi waheshimu utashi wa wananchi wa Zambia na uhuru wao wa
kikatiba ili waweze kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi mdogo. Viongozi wa
kidini hawana budi kuachana na tabia ya kuwaalika baadhi ya wagombea Urais kutumia
nyumba za Ibada kama majukwaa ya kisiasa, jambo linaloweza kuhatarisha amani na utulivu!
Vyama vya kiraia viwahamasishe wananchi wote kushiriki kikamilifu katika uchaguzi
mdogo na kwamba, Tume ya Uchaguzi nchini Zambia haina budi kuhakikisha kwamba, kweli
uchaguzi unakuwa huru na wa haki; vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe kwamba,
kuna amani na utulivu.