2014-12-06 10:35:43

Injili ijikite katika historia na tamaduni za watu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia linaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu lilipoanzishwa, tukio ambalo limebarikiwa kwa uwepo wa Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki ambaye, tarehe 5 Desemba 2014 alipata nafasi ya kuzungumza na Maaskofu Katoliki Ethiopia kwa kuwashukuru katika kukoleza na kuendeleza majadiliano pamoja na kutambua kwamba, hata katika tofauti zilizopo ndani ya Kanisa Katoliki, lakini wote wanaunda Kanisa, moja takatifu, katoliki na la mitume!

Kardinali Sandri amewasilisha salamu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Ethiopia, kwani kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa sanjari na huduma ya mapendo inayotolewa na Mama Kanisa kwa watoto wake, yote haya yanafumbatwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya mapungufu ya kibinadamu kwani hii ni kazi iliyofanywa na Mababa wa Kanisa tangu mwanzo wa Ukristo.

Injili ya Kristo imeota mizizi yake nchini Ethiopia hata kama Wakatoliki bado ni idadi ndogo nchini humo, changamoto ya kuendeleza moyo wa kiekumene ili kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, kwa kuendelea kuwa ni mashahidi hai wa Mapokeo ya Kitume.

Kama wafuasi wa Kristo wamepakwa mafuta na wanatumwa tena na Roho Mtakatifu kwenda kutangaza Injili ya Furaha kwa Watu wa Mataifa na kwamba, hii ni dhamana inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, ili kweli Injili iweze kujikita katika historia na tamaduni za watu, lakini wote wakitambua kwamba ni ndugu zake Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

Maaskofu katika dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu hawana budi kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaongoza Watu wao pamoja na kuendeleza mshikamano na umoja wa Kanisa kwa njia ya: majiundo awali na endelevu; utume kwa vijana, ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; Katekesi ya kina inayojichimbia katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala; Elimu na huduma za afya kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki litaendelea kufadhili miradi mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ethiopia, bila kusahau kushiriki katika mchakato wa msamaha na upatanisho, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu kati ya wananchi wa Ethiopia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.