2014-12-06 15:54:14

Huruma, upendo na mshikamano ndiyo ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2014


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 6 Desemba 2014 ametembelea Hospitali ya Bambino Gesù inamilikiwa na kuendeshwa na Vatican, ili kuwasalimia watoto waliolazwa Hospitalini hapo pamoja na kuwatakia kheri na baraka kwa ajili ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka mpya wa 2015. Kardinali Parolin alipowasili Hospitalini hapo amepokelewa na viongozi wakuu wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na kuzungumza na wazazi na watoto wagonjwa waliolazwa Hospitalini hapo.

Kardinali Parolin akiwa ameambatana na viongozi wa Hospitali ya Bambino Gesù ametembelea idara ya huduma kwa watoto mahututi waliofanyiwa upasuaji wa moyo; sehemu ambayo hivi karibuni ilifanyiwa ukarabati mkubwa, ili kuiwezesha Hospitali kutoa huduma makini kwa watoto wanaotoka sehemu mbali mbali za dunia. Itakumbukwa kwamba, hata watoto kutoka Tanzania kwa miaka kadhaa walikuwa wanapata tiba ya magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, iliyoko Itigi, Singida, Tanzania.

Baadaye Kardinali Parolin amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wagonjwa, wafanyakazi na watu wanaojitolea kutoa huduma mbali mbali hospitalini hapo na kuwashukuru kwa moyo wao wa upendo, ukarimu na mshikamano, uliowezesha Hospitali ya Bambino Gesù kutoa huduma kwa familia 4500, karibu ya watu 13, 500 pamoja na huduma kwa watu zaidi ya 102, 000 waliohudumiwa katika majengo ya Hospitali ya Bambino Gesù.

Kardinali Parolin amewashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoitekeleza kwa niaba ya Mama Kanisa miongoni mwa watoto wadogo, kwa kuwaonjesha upendo, ukarimu na mshikamano mambo muhimu yanayousukuma ulimwengu kusonga mbele kwa imani na matumaini, licha ya mapungufu ya kibinadamu. Huduma zinazotolewa Hospitalini hapo zinawawezesha wazazi na watoto wagonjwa kuishi katika mazingira bora yanayoheshimu na kujali utu wa binadamu, changamoto ya kuendelea kuwamegea watu upendo huu siku kwa siku. Kardinali Parolin anasema, huu ndio ujumbe na matashi mema ya Noeli kwa Mwaka 2014.

Kardinali Parolin ametembelea na kusali kidogo kwenye Kikanisa cha Hospitali ya Bambino Gesù kilichojengwa kunako mwaka 1869 na Familia ya Salviati waliotoa zawadi kwa Vatican kunako mwaka 1924. Kikanisa hiki kinahifadhi masalia ya Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II. Kabla ya kurejea mjini Vatican, Kardinali Parolin amewatembelea wagonjwa waliolazwa kwenye wodi ya mfumo wa chakula, eneo ambalo pia linatoa huduma kwa wagonjwa wenye magonjwa nasibu.All the contents on this site are copyrighted ©.