2014-12-06 12:18:04

Hija ya haki na amani duniani!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuendeleza hija ya kiekumene kwa kuwa na mwelekeo mpya, huku likijitahidi kutumia fursa mbali mbali zinazojitokeza, ili kumwilisha dhana hii katika uhalisia wa maisha na utume wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, kwa kuongozwa na kauli mbiu “hija ya haki na amani, mwono uliotolewa kwenye mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ulioadhimishwa Korea ya Kusini, Desemba 2013. RealAudioMP3

Akitafakari kuhusu changamoto hii, Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, Makanisa Ulimwenguni hayana budi kusonga mbele kwani dunia inaendelea kucharuka, kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kutumia fursa mbali mbali zinazojitokeza, ili kuwaendea wale walioko pembezoni mwa jamii. Baraza la Makanisa Ulimwenguni halina budi kuendelea kujikita katika mchakato wa kuimarisha umoja na mshikamano na Makanisa mbali mbali, ili kuwatangazia vijana wa kizazi kipya Habari Njema ya Wokovu.

Dr. Tveit ameyasema haya hivi karibuni alipokuwa anazungumza kwenye Mkutano wa Kamati kuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, iliyokutana huko Paralimni, Cyprus. Kamati kuu imefanya mkutano huu nchini Cyprus, mahali ambapo watu wengi wanaendelea kuteseka kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Ni watu wanaohitaji kuonjeshwa moyo wa upendo na mshikamano, bila kuwasahau Wakristo wanaoendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Umoja na mshikamano ni nyenzo muhimu sana katika kuwahudumiwa walimwengu pamoja na kujibu kilio cha watu wote wanaoteseka kutokana na ukosefu wa misingi ya haki, amani na utulivu. Umoja na mshikamano wa kiimani ni ushuhuda mkubwa wenye mvuto na mashiko kwa watu wengi duniani. Cyprus ni kitovu cha mshikamano na wahamiaji pamoja na wageni wanaotafuta nafuu ya maisha Barani Ulaya.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mpango kazi wake, linapania kuendelea kuhimiza misingi ya haki na amani huko Syria, Iraq, Ukraine, Korea ya Kusini na Kaskazini; Israeli na Palestina, Nigeria, Sudan ya Kusini na huko DRC. Hizi ni nchi ambazo zinahitaji kwa namna ya pekee amani na utulivu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kuhamasisha umuhimu wa jamii za watu kuzingatia misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu. Baraza la Makanisa pia linapenda kusimama kidete kuchangia katika dhana ya utunzaji bora wa mazingira, kwa kushirikisha Umoja wa Mataifa, mawazo na changamoto zao.

Baraza la Makanisa Ulimwengu litaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu; utoaji wa msaada wa dharura, kusimamia haki msingi za binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na haki sawa katika masuala ya tabianchi, bila kusahau mchango wa Makanisa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na Ebola ambao kwa sasa limekuwa ni janga la kimataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni litaendelea kukuza na kudumisha umoja na Kanisa Katoliki, ambalo kimsingi si mwanachama wa Baraza hili, lakini limekuwa likishiriki kikamilifu katika mikutano na mikakati yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.