2014-12-06 10:43:34

Bado amani na usalama viko hatarini!


Mawaziri wa Shirikisho la Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, OSCE wamehitimisha mkutano wao wa ishirini na moja, wakati ambapo vita, kinzani, vitendo vya kigaidi na hali ya kukata tamaa kutokana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, uhuru pamoja na watu wengi kuendelea kupoteza maisha na kwamba, utu na heshima ya binadamu viko mashakani.

Licha ya kasoro zote hizi, OSCE imeshindwa kuzuia na kudhibiti masuala haya, changamoto kwa ncghi wanachama kuhakikisha kwamba, zinatekeleza: itifaki, maazimio na sheria zilizopo ili kuzuia vita na kinzani za kijamii. Ni jambo la kusikitisha sana kuona kwamba, watu wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita, mshikamano wa dhati unapaswa kuoneshwa kwa wale wote ambao wanakabiliwa na majanga haya, kiasi cha kuwanyima uhuru wa kuishi katika amani na utulivu.

Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Dominique Mamberti aliyekuwa Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati akichangia hoja kwenye mkutano wa Mawaziri wa OSCE, uliokuwa unafanyika mjini Basel, Usswis. Anasema, kuna haja ya kuondokana na tabia ya kutumia silaha kama suluhu ya matatizo yanayojitokeza ndani ya jamii na badala yake watu wajenge tabia na utamduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu.

Umefika wakati wa kuachana na falsafa ya kulipizana kisasi na kuanza mchakato wa majadiliano yanayojikita katika msamaha na upatanisho wa kweli, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, kuaminiana na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko. Majadiliano ndiyo njia muafaka ya kuweza kupata suluhu ya kinzani na migogoro ya kimataifa, ili kudumisha amani na utulivu.

Askofu mkuu Dominique Mamberti anasema, mkutano wa OSCE umefanyika wakati Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Jubilee ya miaka mia moja tangu Vita kuu ya Kwanza ya Dunia ilipotokea na miaka sabini na mitano tangu Vita kuu ya Pili ya Dunia ilipofumuka na kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na falsafa na kampeni zinazotaka kukuza na kuendeleza sera za ubaguzi, mambo yanayohatarisha amani, uhuru na utulivu kwani amani ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka ishirini na mitano tangu Ukuta wa Berlin ulipoangushwa, alama ya chuki na uhasama uliopitwa na wakati na kwamba, Jamii kwa sasa inahamasishwa kujenga matumaini kwa kutambua kwamba, inawezekana kushinda vikwazo na hivyo kudumisha utu na heshima ya binadamu, kwa kukazia: usalama, amani na utulivu.

Uvunjifu wa haki msingi za binadamu, utu na heshima yake ni mambo yanayohatarisha ulinzi na usalama katika nchi za OSCE, mwaliko kwa nchi wanachama kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha haki msingi za binadamu; kwa kusimama kidete kupinga biashara haramu ya binadamu ambayo kwa sasa ni tishio kubwa kwa utu na heshima ya binadamu.

Uhuru wa kuabudu ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwani kunaendelea kuibuka misimamo mikali ya kidini inayoambatana na vitendo vya kigaidi, mambo yanayohatarisha amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Maisha ya mwanadamu hayana budi kulindwa na kudumishwa, kwani hii ni haki ya kwanza kabisa ambayo mwanadamu anapaswa kuhakikishiwa.

Vatican haiwezi kukaa kimya na kuona kwamba, kuna maelfu ya watu wanaouwawa, wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao; mambo ambayo hayana budi kulaaniwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. OSCE haina budi kutekeleza wajibu wake pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam, ili kweli amani ya kweli iweze kupatikana, sanjari na uhuru wa kuabudu, kwani vitendo vyovyote vile vinavyovunja uhuru wa kuabudu vinahatarisha amani na usalama wa raia na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.