2014-12-05 08:27:40

Nguvu ya imani inawawezesha Wakristo huko Mashariki ya Kati kuvumilia kwa saburi!


Wakristo Mashariki ya Kati wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na nyanyaso na madhulumu ya kidini, lakini wanaweza kusonga mbele kwa imani na matumaini kutokana na mshikamano unaonesha na Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama nguvu inayoweza kuwaokoa Wakristo huko Mashariki ya Kati. Mshikamano wa kidugu umekuwa ni utambulisho mkubwa unaotolewa na Wakristo wanaounga mkono maisha na utume wa Kanisa katika Nchi Takatifu.

Ukristo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya watu huko Mashariki ya Kati na kwamba, Wakristo licha ya changamoto na magumu wanayokabiliana nayo bado wana dhamana ya kuendelea kuishi katika Nchi Takatifu kwani wao pia ni utambulisho wa Mashariki ya Kati. NI maneno ya Padre Pierbattista Pizzaballa, Mlinzi mkuu katika Nchi Takatifu, alipokuwa anazungumza hivi karibuni na Jumuiya za Kikristo huko Yerusalemu, wakati huu wa Kipindi cha Majilio, kipindi cha kukuza na kuimarisha, imani, matumaini na mapendo.

Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia wataendelea kuonesha mshikamano wao katika maisha ya kiroho kwa njia ya sala, kimaadili pamoja na kuwajengea uwezo ili kukabiliana na changamoto za maisha, huku wakiendelea kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Nyanyaso na madhulumu ya kidini huko Iraq na Syria yanahitaji mshikamano wa sala na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani sanjari na Maadhimisho ya Kipindi cha Majilio ni nafasi murua kabisa kwa Wakristo huko Mashariki kukutana na kuadhimisha kwa pamoja Mafumbo ya Kanisa, kwa kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha ya kila siku. Mwaka wa Watawa ni nafasi kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kinabii kwa kuwaonjesha waamini: imani, furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Majilio ni kipindi cha kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, kwa kuwaonjesha wengine mshikamano kama ambavyo unajionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Uwepo wa Watawa katika Nchi Takatifu ni kuendelea kushuhudia kwamba, Yesu Kristo aliyependa kuzaliwa katika Nchi Takatifu bado yupo kati ya watu wake kwa njia ya Watawa wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Watawa kwa njia ya maisha na utume wao, wanajitahidi kumpeleka Kristo kwa jirani zao kwa njia ya ushuhuda wa huduma makini inayotolewa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Watawa wanashirikisha karama mbali mbali za maisha na utume wao, kielelezo kinachoonesha utajiri mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Tofauti za karama ni mwaliko wa kumwilisha upendo wa Mungu kati ya watu wake, ili waendelee kuwa na imani, mapendo na matumaini thabiti katika maisha yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.