2014-12-05 07:59:08

Mchakato wa Uinjilishaji Barani Asia ni changamoto kwa Kanisa Barani Asia


Utume wa Kanisa Barani Asia ndiyo mada iliyochambuliwa hivi karibuni katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Shirika la Habari za Kanisa Barani Asia, “Asianews” na kuadhimishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa kongamano hili, amewataka wahusika kuamsha tena ari na shahuku ya kutaka kuzama zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji Barani Asia. RealAudioMP3

Huu ni mwendelezo wa changamoto ya Uinjilishaji inayotolewa na Mababa wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, utume ambao ulifunguliwa rasmi na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1995, na baadaye Baba Mtakatifu Francisko, mwezi Agosti, 2014 akafanya hija yake ya kichungaji nchini Korea.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kutoka huko lilikojificha na kuwaendea watu wanaoishi pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha, ili wao pia waweze kuonja huruma, upendo na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa. Mwelekeo huu unajionesha katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye mwanzoni mwa Mwaka 2015 anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji nchini Sri Lanka na Ufilippini, ili kuwaimarisha ndugu zake katika Kristo kwa kuwaonjesha huruma na upendo na mshikamano kutoka kwa Kristo.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini anabainisha kwamba, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwake, inaongozwa na kauli mbiu ni “huruma na wema”, ili kuwagusa watu ambao wameathirika vibaya kutokana na tufani ya, matetemeko ya ardhi; madhara ya rushwa na ufisadi wa fedha na mali ya umma; maskini, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Hija hii inapania kuamsha tena dhamiri nyofu miongoni mwa wananchi wa Ufilippini. Ni huruma inayopaswa kutolewa pia kwa maelfu ya wananchi wanaoishi kandoni mwa Bara la Asia. Ikumbukwe kwamba, Wakristo Barani Asia wanaunda kundi dogo sana, ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine; hapa ni mahali ambapo Injili inatangazwa kwa njia ya mchakato wa majadiliano. Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea ya Kusini, iliwagusa wengi na kuwaacha wameshikwa na bumbuwazi.

Wakristo wanaishi katika mazingira magumu kutokana na baadhi ya waamini kuwa na misimamo mikali ya kiimani, inayogumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Kuibuka kwa kasi kubwa kwa vitendo vya kigaidi kunatishia amani na usalama huko Mashariki ya Kati anasema Patriaki Louis Raphael Sako kutoka Baghdad. Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea katika maeneo kama haya, anakuwa kweli ni faraja na changamoto ya matumaini kwa Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Si rahisi kwamba, Wakristo waliokimbia makazi yao wanaweza kurejea mapema hivi, bali itawachukua siku kadhaa hadi hali iweze kurejea tena kama ilivyokuwa, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashikamana kupinga biashara ya silaha pamoja na kusitisha ufadhili kwa vikundi vya kigaidi vinavyoendelea kupandikiza mbegu ya chuki na maafa kwa watu wasiokuwa na hatia.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, Uinjilishaji Barani Asia ni changamoto kubwa kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, changamoto ambayo kwa sasa inavaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuanza kutembelea nchi kadhaa za Bara la Asia. Ikumbukwe kwamba, kila siku ni siku ya Bwana, ni matumaini ya Kanisa Barani Asia kwamba, Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai ataweza kubariki juhudi hizi za kimissionari Barani Asia katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.