2014-12-05 09:06:22

Kipindi cha Majilio!


Mhariri wa Jarida "La Cività Cattolica" anawaalika wasomaji wake katika kipindi hiki cha Majilio kutafakari kwa kina na mapana baadhi ya mahubiri yaliyowahi kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika utume na maisha yake kwa kuangalia mwanga wa Noeli, ili waamini waweze kuwa kweli ni watoto wa mwanga unaowaamsha kufikiri na kutenda kama Watoto wa Mungu.

Mwana wa Mungu ambaye alifanyika Mwanga ili kufukuza giza katika maisha ya mwanadamu si mwanga unaotisha, lakini ni angavu na uko karibu sana na maisha ya mwanadamu. Huu ni mwanga unaochochea toba na wongofu wa ndani katika maisha ya mwamini, ili kamwe asimezwe na malimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwa kweli ni Watoto wa Mwanga, ili waweze kutembea katika mwanga wa utakatifu wa maisha, mwaliko wa kwanza kwa kila Mkristo, kwani wanapomwona Mtoto Yesu akiwa amelazwa kwenye Pango la kulishia wanyama, hapo wanaweza kuonja ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Mwanga unaoletwa na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili unawamsha waamini kutoka katika usingizi, ili kuwasaidia kutembelea katika dunia hii kwa moyo wa unyenyekevu, huku wakiendelea kukua na kuongezeka katika kimo na busara kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Majilio na hatimaye Siku kuu ya Noeli ni kipindi cha matumaini na mwanzo wa maisha mapya yanayojikita katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu ni mwendelezo wa mchakato wa majiundo endelevu katika azma ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo.

Katika kipindi cha Majilio, Mama Kanisa anapenda kumwonesha kwa namna ya pekee Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu, aliyejitaabisha kuhakikisha kwamba, Familia Takatifu inapata mahitaji yake msingi, huku akijiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumwongoza kadiri ya mpango na haki yake ya Kimungu, tofauti kabisa na haki ambayo wakati mwingine binadamu anapenda kumsingizia Mungu, changamoto kwa Wakristo kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao.

Yesu alizaliwa mjini Bethelehemu, Nyumba ya Mkate, pembezoni mwa Utawala wa Kirumi, ndivyo Mwenyezi Mungu katika Fumbo la Umwilisho, amependa kujinyenyekesha na kuzaliwa kama binadamu, lakini zaidi katika Pango la kulishia wanyama. Noeli ni Siku kuu inayoonesha ukuu na utukufu wa Mungu katika mambo ya kawaida. Hapa mwamini anajifunza kwamba, Mwenyezi Mungu anatekeleza mpango wa ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya Fumbo la Umwilisho.







All the contents on this site are copyrighted ©.