2014-12-05 12:23:24

Familia ni mhimili mkuu katika ustawi na maendeleo ya Jamii na Kanisa!


Ekolojia ya maisha ya mwanadamu na fursa ya kazi ni mambo muhimu katika mchakato unaopania kukuza na kudumisha maendeleo ya kiuchumi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia. Kwa maneno haya, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 5 Desemba 2014 ametuma ujumbe kwa washiriki wa Tamasha la Familia kwenye Manispaa ya Riva del Garda iliyoko Trento, Kaskazini mwa Italia na kusomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Luigi Bressan wa Jimbo kuu la Trento.

Tamasha la Familia ambalo limeingia katika awamu ya tatu kwa mwaka 2014, linawashirikisha wadau mbali mbali wanaotetea misingi bora ya maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, familia ni msingi wa jamii na Kanisa na kwamba, maendeleo ya binadamu yanapitia katika familia, inayopaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Haki msingi za familia zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa mintarafu mahusiano ya kitaaluma na maisha ya kifamilia.

Baba Mtakatifu anasema familia inawajibika kutoa huduma kwa wanajumuiya wake, ili kukuza na kudumisha maisha na kwamba, ina haki zake msingi na wajibu unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, ili kweli familia ziweze kutoa mchango wake katika ustawi na maendeleo ya binadamu kwa kujikita katika mshikamano unaongozwa na kanuni auni; malezi na majiundo kwa watoto; mambo yanayohitaji ushirikiano wa dhati.

Baba Mtakatifu anasema, kutokana na kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa, kuna haja ya kuibua mbinu mkakati utakaotekelezwa na jamii kwa kuonesha ujasiri wa kulinda familia; cheche za maendeleo ya kiuchumi. Jamii haina budi kulivalia njuga tatizo la ukosefu wa ajira hususan miongoni mwa vijana, kwani linawafanya vijana wengi kukosa amani na utulivu; kunachangia jamii kudidimia katika lindi la umaskini na hivyo kukosa nguvu kazi ambayo ingeweza kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi.

Sera makini za familia ni muhimu sana katika kuunga mkono tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kihali na kimaadili. Kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa upatikanaji wa fursa za ajira kwa wanawake, kwa kutambua na kuheshimu haki zao msingi na huduma wanazotoa katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii na kitaaluma bila kusahau mchango wao katika familia na jamii kwa ujumla. Wanawake wengi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao bila kutambuliwa wala kusaidiwa.

Kumbe, anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya wanawake kuangaliwa kwa makini wasifanye kazi ngumu sana zinazowanyima nafasi ya kutekeleza wajibu wao ndani ya familia pamoja na kutoa malezi kwa watoto wao. Kazi zinazofanywa na wanawake ndani ya familia zinapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa na jamii, kwani zinalenga ustawi na maendeleo ya jamii husika.All the contents on this site are copyrighted ©.