2014-12-05 07:52:20

Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya matumaini na mkate wa unaozima kiu ya maisha ya kiroho!


Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalozima kiu ya maisha ya kiroho kwa mwamini na hivyo kumkirimia nguvu ya kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo. Ekaristi Takatifu inaonesha uwamo wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai, mwamba thabiti wa imani, kwa mwamini anayethubutu kumkimbilia Yesu, ili kumwabudu, kumwomba na kumsujudu katika maisha yake. RealAudioMP3

Kipindi cha Majilio ni nafasi murua ya kutambua uwepo endelevu wa Kristo katika hija ya maisha ya waamini na kwamba, kipindi hiki mara nyingi kinahusishwa na maandalizi ya Siku kuu ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa Dunia. Yote haya ni kweli, lakini, Kipindi cha Majilio ni mwaliko kwa waamini kuvunja tabia ya mazoea katika masuala ya kidini na kuanza kujikita zaidi katika imani inayowaonesha uwepo wa Mungu kati yao, changamoto ya kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha, kwani Mungu yupo pamoja na watu wake.

Hivi ndivyo Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi wa Jimbo kuu la Roma anavyowaandikia wanafunzi Wakristo wanaosoma katika taasisi za elimu na vyuo vikuu mjini Roma katika kipindi hiki cha Majilio. Imani inapata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ndiyo maana Mama Kanisa anawakumbusha waamini kwamba, Neno wa Mungu, aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, ndiye Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, aliyezaliwa duniani yapata miaka elfu mbili iliyopita.

Yesu Kristo yupo ndani ya Kanisa lake kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Yesu atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Waamini wanatambua kwamba, Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, “Nyumba ya Mkate”, yeye ndiye sababu ya matumaini yasiyodanganya kamwe, kwani atawawezesha waamini kufikia utimilifu wa maisha.

Askofu msaidizi Leuzzi anawakumbusha wanafunzi kwamba, kwa bahati mbaya wakristo nao wamekumbwa na “ugonjwa wa kukosa uvumilivu” ni watu wenye haraka zao, hawana tena subira, wanapelekwa mchakamchaka na maendeleo ya sayansi na utandawazi kana kwamba, ni daladala iliyokatika usukani. Ndiyo maana, Kipindi cha Majilio, kinawaalika waamini kuvuta subir a pamoja na kuwa na matumaini, huku wakimwomba, Yesu kuwapatia chakula cha uzima wa milele, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni.

Huu ni Mkate wa matumaini, unaowachangamotisha waamini kuwa imara na thabiti katika imani, matumaini na mapendo! Kusimika maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake bila ya kuyumba wala kuyumbishwa, kwani inapendeza na inalipa kumtumainia Yesu Kristo! Waamini wanaalikwa kumkimbilia Yesu, ili aweze kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho na kuwaimarisha katika imani, tayari kuishuhudia katika uhalisia wa maisha, kwa kuwakirimia furaha na maisha ya uzima wa milele. Yesu ni dira na mwongozo thabiti wa maisha.

Kipindi cha Majilio, iwe ni fursa makini ya kujiandaa kwa ajili ya kumpokea Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, Yesu Kristo, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, kwani maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli si kukumbuka mambo ya kale, lakini ni Siku kuu inayoonesha uwepo endelevu wa Yesu Kristo Mwana wa Mungu kati ya watu wake; Yesu ambaye atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kujitahidi kupokea Mkate wa uzima, unaozima kiu ya maisha ya uzima wa milele, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.