Biashara haramu ya binadamu inadharirisha utu na heshima ya binadamu!
Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wadau mbali mbali wanaoshiriki katika mkutano
wa kimataifa wa kupambana na biashara haramu ya binadamu, unaofanyika mjini London,
Uingereza kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 6 Desemba 2014. Hizi ni juhudi zinazopania
kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kisheria ili kupambana na biashara haramu ya
binadamu sanjari na kuwasaidia waathirika wa biashara hii.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu
uliotumwa kwa Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza
na Wales, umesomwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko na Askofu Marcelo Sanchez
Sorondo, Mkuu wa Taasisi za Kipapa za Sayansi Jamii, anayeshiriki katika mkutano huu
wa kimataifa unaowajumuisha Maaskofu, Wakuu wa Jeshi la Polisi nchini Uingereza pamoja
na Kikundi cha Santa Marta, kilichoanza utume wake mjini Vatican, Mwezi Aprili 2014.
Baba
Mtakatifu anasema, biashara haramu ya binadamu ina dharirisha utu na heshima ya binadamu
na kwamba, anawashukuru wadau wote wanaojipanga barabara kuhakikisha kwamba, wanalivalia
njuga tatizo hili la biashara haramu ya binadamu na kwamba, Kanisa litaendelea kuwa
mstari wa mbele katika mapambano haya.