2014-12-04 07:48:21

Zingatieni kanuni maadili kujikwamua na myumbo wa uchumi kimataifa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika mkutano wake wa mwaka uliofanyika hivi karibuni, uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “Kanisa katika huduma kwa Maskini”, limetafakari kwa kina hali na mahangaiko ya wananchi wengi wa Hispania kutokana na madhara ya myumbo wa uchumi kimataifa na kuwataka wadau mbali mbali kutenda kwa kuzingatia kanuni msingi za kimaadili na utu wema. RealAudioMP3
Kuna makosa makubwa ya kiufundi ambayo yamefanywa na wanasiasa, wachumi na watunga sera, kiasi cha kuwakatisha wananchi tamaa kutokana na misigano na kinzani za kijamii zinazojitokeza nchini humo.

Hii inatokana na ukweli kwamba, pengo kati ya maskini na matajiri linaendelea kuongezeka kila kukicha, kiasi kwamba, hali hii inaanza kusababisha kinzani za kijamii. Ukuaji wa uchumi hauna budi kuzingatia usawa na maendeleo ya watu kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na matumizi na mgawanyo sawa wa rasilimali ya nchi, kuliko baadhi ya watu ndani ya jamii kufaidika na matunda ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, wakati wengine wakiendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato!

Maaskofu Katoliki Hispania wanasema, licha ya sera na mikakati makini ya kiuchumi inayopangwa na Serikali, lakini kuna haja kwanza kabisa ya kujipyaisha tena katika kanuni maadili kwa kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake; ili kujenga misingi ya ukweli na uwazi; uaminifu na hekima; heshima na kuwajali wengine; mafao ya wengi na ustawi wa wote pamoja na mashikamano wa dhati miongoni mwa wananchi, vinginevyo nchi itaendelea kuporomoka katika medani mbali mbali za maisha, kiasi cha kuhatarisha demokrasia.

Maaskofu Katoliki Hispania wanasema kwamba, maendeleo ya kisiasa yanapata chimbuko lake katika demokrasia ya kweli inayoheshimu na kuthamini utawala wa sheria, haki msingi za binadamu pamoja na utu wa binadamu. Ni wajibu na dhamana ya Serikali kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau mbali mbali katika kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia badala ya mtindo wa sasa wa Serikali kuonekana kuwa ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya familia, kwani familia ni shule ya Injili ya uhai na kiini cha jamii.

Upendo wa kweli na mshikamano wa dhati kati ya Bwana na Bibi ni chemchemi ya Injili ya Uhai; Utu na heshima ya binadamu katika hatua za maisha yake, kama kielelezo cha jamii inayosimikwa katika haki, amani na uhuru wa kweli.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linajiandaa kuadhimisha Jubilee ya miaka mia tano tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Theresa wa Avilla, tukio ambalo linatarajiwa kuwakutanisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 9 Agosti 2015 huko mjini Avilla, Hispania.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wananchi wote wanaoteseka kutoka na baa la umaskini; wahamiaji, watu wasiokuwa na fursa za ajira na kwa namna ya pekee kabisa vijana. Maaskofu wanawashukuru na kuwapongeza waamini na wananchi ambao wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya kuonesha upendo na mshikamano kati ya watu na hasa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.