2014-12-04 07:42:54

Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani!


Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri mkuu wa nyumba ya kipapa, kuanzia Ijumaa ya tarehe 5 Desemba 2014 ataanza kutoa mahubiri ya kipindi cha Majilio kwa Baba Mtakatifu Francisko na viongozi wengine wa Kanisa wanaoishi mjini Roma. Mwaka huu, Padre Cantalamessa anasema, mahubiri yake yatajikita katika “Amani na Mwenyezi Mungu ndiyo inayojenga mahusiano mema ya kibinadamu”. RealAudioMP3

Mahubiri haya yatatolewa kwenye Kikanisa cha Mama wa Mkombozi, kilichoko mjini Vatican. Mahubiri haya yataongozwa kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka, sura ya 2: 14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia”. Hii ni tema muhimu sana kwa wakati huu ambako mtutu wa bunduki unaendelea kurindima sehemu mbali mbali za dunia na kusahau kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha binadamu.

Umefika wakati kutoa maana ya kina ya neno “Amani” na baadaye kuendelea kusikiliza ujumbe wa kuzaliwa kwa Mkombozi na Mfalme wa amani duniani, huku waamini wakiwa na mwelekeo mpya wa maisha, tayari kumwilisha ujumbe wa siku ya kuombea amani duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari, sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” kama inavyojulikana tangu awali na Mababa wa Kanisa.

Ijumaa ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, Padre Cantalamessa anasema kwamba, atafanya tafakari ya kina kuhusu amani kama zawadi kutoka kwa Yesu Kristo, zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anamkirimia mwanadamu, hali inayojionesha katika kazi ya Uumbaji.

Pale mwanadamu anapojitahidi kujenga na kudumisha amani na Mwenyezi Mungu anaweza kupata pia amani ndani mwake na kati ya watu wanaomzunguka; amani inadumishwa kati ya binadamu na mazingira yake. Lakini, kunapatashika nguo kuchanika, ikiwa kama mwanadamu atashindwa kujenga na kudumisha amani na Mwenyezi Mungu, matokeo yake ni kinzani kati ya Adamu na Eva, kati ya mtu na mtu na haya ndiyo yanayosimuliwa kwenye Kitabu cha Mwanzo.

Mwanadamu anaweza kuweka sahihi ya mkataba wa amani, lakini hakupatikani na amani ya kweli, hadi pale mahusiano ya dhati yatakapojengwa na Mwenyezi Mungu, matokeo yake ni watu daima kupenda kurudi msituni! Amani ya kweli inajikita kwa kutambua ukuu na wema wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Kwa waamini anasema Padre Cantalamessa, amani hii inapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya watu. Mahusiano haya ni muhimu hata katika mahusiano ya kitamaduni kwa watu mamboleo, vinginevyo, watu wataogelea katika utupu, kinzani na migongano ya kivita.

Ijumaa ya Pili ya Kipindi cha Majilio, tarehe 12 Desemba 2014: Tafakari itajikita katika Amani kama wajibu na dhamana inayopaswa kufanyiwa kazi. Hapa waamini wanaalikwa kujichotea utajiri kutoka katika muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu, juu ya Heri za Mlimani, yaani … Heri wapatanishi. Hapa Padre Cantalamessa anasema, halengi kuzungumzia masuala ya kisiasa kwani huu kwa sasa ni wimbo usiokuwa na kiitikio.

Hapa mkazo ni kuona jinsi gani Yesu alivyowafundisha Wafuasi wake kupata amani ya kweli na inayodumu. Ni wakati wa kuangalia umuhimu wa dini mbali mbali kujenga na kudumisha misingi ya amani, kwa kukazia amani na majirani bila kusahau kwamba, hata Watoto wa Kanisa wanapaswa kutawaliwa na misingi ya amani, kwa kujenga na kukuza umoja, mshikamano na udugu ndani ya Kanisa.

Ijumaa ya tatu ya Kipindi cha Majilio: tarehe 19 Desemba 2014, tafakari itajikita katika amani kama zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu, anayemwezesha mwamini kupata utulivu wa ndani. Padre Cantalamessa anasema, mahubiri ya Kipindi cha Majilio yanalenga kwa namna ya pekee kuwasaidia viongozi wa Kanisa katika safari ya maisha yao ya kiroho, ili kuwajalia kuwa na amani na utulivu wanapotekeleza dhamana na majukumu yao ya kila siku. Amani ya kweli inapatikana kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.