2014-12-04 14:48:57

Rais Guebuza wa Msumbiji akutana na Baba Mtakatifu mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 4 Desemba 2014 amekutana na kuzungumza na Rais Armando Emìlio Guebuza wa Msumbiji ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya viongozi hawa wawili, wamefurahishwa na mahusiano mazuri kati ya nchi hizi mbili. Wamepongeza mchango unaotolewa na Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Msumbiji, kwa kutumia taasisi zake zinazotoa huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Kanisa limechangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa kukuza na kudumisha amani na upatanisho wa kitaifa nchini Msumbiji.

Mwishoni, Baba Mtakatifu na mgeni wake wamezungumzia masuala ya kikanda na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti biashara ya silaha ambazo zimekuwa ni chanzo cha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi, umaskini na ukosefu wa usawa kati ya watu. Rais Guebuza na ujumbe wake wametembelea na kuzungumza na waandishi wa Habari za Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.