2014-12-04 08:02:59

Neno la Mungu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Galles limejiwekea mikakati ya kichungaji kwa ajili ya Kipindi cha Majilio, ili kuwahamasisha waamini kusoma, kusikiliza, kutafakari na kulitangaza Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. RealAudioMP3

Kwa namna ya pekee, mkazo umewekwa tarehe 7 Desemba 2014, Jumapili ya pili ya Kipindi cha Majilio, kipindi cha matumaini, wakati ambapo waamini wanasubiri kwa hamu kubwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliwahimiza waamini kujikita katika kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao kama kielelezo cha imani tendaji, kwani Kristo ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu kwa watu wake. Ni wajibu na dhamana ya Kanisa kuhakikisha kwamba, inawarithisha waamini utajiri wa Neno la Mungu, kwa kufuata Mapokeo Matakatifu kwa kutambua kwamba, Biblia Takatifu imeandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, kwa kumshirikisha mwanadamu hekima ya Kimungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linasema kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wa Kitume, Neno la Mungu, “Verbum domini” anawaalika waamini kusoma Neno la Mungu kwa umakini mkubwa bila ya kuchoka, kwani kwa njia hii, wataweza kumfahamu Yesu Kristo sanjari na kukabiliana na changamoto za maisha kwa msaada wa Neno la Mungu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo, Waamini walisome Neno la Mungu kwa furaha na uchaji mkubwa pamoja na kujiundia mazingira ya sala, ili Mwenyezi Mungu na binadamu waweze kuongea kwa pamoja, kwani wanaongea na Mungu wakati wa sala au wanaposikiliza kwa makini Neno la Mungu likitangazwa mbele yao.

Jumapili ya Neno la Mungu ni mwaliko na changamoto kwa Waamini kuvumbua mbinu mpya inayobubujika kutoka kwenye Neno la Mungu, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa kujikita katika Neno la Mungu. Lengo ni kuinjilisha na kuimarisha Katekesi, ili waamini waweze kukiri Imani, Kuiadhimisha, Kuimwilisha na Kuisali.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Galles, kwa kushirikiana na Chama cha Biblia Uingereza wanasema kwamba kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa kungojea kuzaliwa kwa Masiha, ni wakati wa kukesha kwa Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma. Waamini wanahimizwa kukuza na kujenga moyo wa kusoma, kusikiliza, kutafakari, kutangaza na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalia wa maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.