2014-12-04 14:46:50

Msiwatumie maskini kujitajirisha!


Shirikisho la vyama vya kujitolea vya Kanisa Katoliki nchini Italia vina mchango mkubwa katika kuwasaidia watu waliokumbwa na majanga mbali mbali duniani, Kanisa kwa upande wake litaendelea kushikamana na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Shirikisho la vyama hivi ni mfano bora wa Wasamaria wema wanaotekeleza dhamana na majukumu yao kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kwa kupambana kikamilifu na baa la njaa na kashfa ya vita duniani.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na Shirikisho la Vyama vya Kujitoleavya Kanisa Katoliki nchini Italia, FOSCIV, Alhamisi, tarehe 4 Desemba 2014 katika maadhimisho ya Siku ya Kujitolea Duniani. Huduma yao ni kielelezo makini cha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu anayeendelea kufanya hija na binadamu katika shida na mahangaiko yake. Kuna haya ya watu kutolea ushuhuda wa sadaka kwa ajili ya maskini, ili waweze kuwa na matumaini yanayofumbatwa katika mshikamano wa upendo. Watu wanaojitolea ni vyombo vya huduma ya Jumuiya inayotolewa kwa ajili ya maskini.

Baba Mtakatifu anasema, haitoshi kuwahudumia maskini tu, bali kujifunga kibwebwe ili kukata mzizi wa fitina unaosababisha baa la umaskini; haya ni mambo yanayojikita katika ukosefu wa usawa, fursa za ajira, makazi; ukosefu wa haki msingi za kijamii na katika maeneo ya kazi. Mshikamano wa upendo na udugu ni njia makini ya kuandika historia mpya na maskini, kwa kulinda na kutunza mazingira, kwani kazi ya uumbaji ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa na kwamba, hii ni hazina inayopaswa kurithishwa kwa kizazi kijacho!

Baba Mtakatifu anasema, bado kuna kashfa ya vita, inayowachangamotisha watu kushikiriana ili kujenga misingi ya haki na amani; kwa kujenga na kuimarisha madaraja ya watu kukutana kidini na kitamaduni, huku wakisindikizwa na imani wanapotekeleza wajibu wao katika mazingira magumu, kwani kazi yao ni kielelezo makini cha amani na matumaini kwa wakimbizi na wahamiaji, wanaokimbia dhuluma na nyanyaso za kidini; watu wanaotafuta maisha bora! Wafuasi wa Kristo wanapaswa kuwasaidia watu hawa kwa kuwaonjesha ukarimu wa Kiinjili badala ya kuwageuzia kisogo.

Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kushirikiana na wadau mbali mbali ili kujenga na kudumisha amani na utulivu kati ya watu wenye tamaduni tofauti, sanjari na kuokoa maisha ya wahamiaji ili wasitumbukie na kufa maji baharini au katika mikono ya wafanyabiashara haramu ya binadamu, watu ambao dhamiri zao zimekufa.

Miaka arobaini ya shughuli za kujitolea si haba anasema Baba Mtakatifu, kwani wamejitahidi kuwa kweli ni mashahidi wa upendo, vyombo vya ujenzi wa haki, amani na mshikamano, mwaliko wa kuendelea kutekeleza utume huu kwa moyo wa furaha unaorutubishwa kwa sala ambayo inawategemeza wakati wanapokumbana na magumu; wanapokata tamaa, wanaposhindwa kueleweka au wanapokumbwa na upweke hasi!

Na Padre Ricard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.