Jeshi la Polisi na Kanisa ni wadau wakuu katika mapambano dhidi ya biashara haramu
ya binadamu inayoendelea kunyanyasa na kufisha utu na heshima ya binadamu. Biashara
hii haramu ni kati ya majanga makubwa yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo
na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya binadamu.
Kwa muda wa siku mbili, kuanzia
tarehe 5 hadi tarehe 6 Desemba, 2014 mjini London, Uingereza kunafanyika mkutano wa
kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu ulioandaliwa na Kikundi cha Santa Marta
kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Jeshi la Polisi nchini
Uingereza. Viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Uingereza wanatarajiwa kushiriki
katika mapambano haya dhidi ya biashara haramu ya binadamu.
Kikundi cha Santa
Marta kilichoanzishwa kunako mwezi Aprili 2014 kinaongozwa na Bwana Bernard Hogan-Howe
pamoja na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza
na Wales, kwa kushirikiana na wakuu wa Majeshi ya Polisi na Maaskofu kutoka sehemu
mbali mbali za dunia; wanaofanya kazi kwa pamoja ili kung'oa biashara haramu ya binadamu
pamoja na kutoa huduma za kichungaji kwa wahanga wa vitendo hivi kwa kinyama.
Kikundi
hiki kinapania pamoja na mambo mengine, kuibua mbinu mkakati wa kuzuia, huduma za
kichungaji pamoja na kushirikiana kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu
ya binadamu.