Tangazeni kwamba, Al Shabaab ni janga la kitaifa Kenya!
Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya ameitaka Serikali ya Kenya kutangaza kwamba, mashambulizi ya Al Shabaab
ni janga la kitaifa pamoja na kufanya udhibiti mkubwa wa uuzaji wa silaha kwa raia,
kama njia ya kupambana na mashambulizi ya kigaidi ambayo yameendelea kusababisha mauaji
ya watu wasiokuwa na hatia kwa misingi ya kidini.
Wananchi wanaendelea kuomboleza
kwa kuondokewa na ndugu, jamaa na rafiki zao, kumbe umefika wakati kwa Serikali kutenda
kwa ujasiri ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kupukutika
kama majani makavu wakati wa kiangazi. Serikali itenge kikosi maalum kitakachokula
sahani moja na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab, kinachofanya mauaji kwa misingi
ya kidini. Serikali inawajibu wa kulinda raia na mali zao na kwamba, kwa sasa maeneo
yaliyoko Kaskazini Mashariki mwa Kenya si salama kwa maisha ya raia na mali zao.
Rushwa
ni chanzo kikuu cha Serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake katika masuala ya ulinzi
na usalama, changamoto kwa Serikali kuhakikisha kwamba, inafanya upembuzi yakinifu
kuhusu watu wanaoteuliwa kufanya kazi katika vyombo vya ulinzi na usalama.