Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka B wa Kanisa
Mpendwa mwana wa Mungu ninakualika katika tafakari ya Neno la Mungu ili polepole ukaze
mwendo katika maandalizi ya kumpokea Mwana wa Mungu. Ni Dominika ya pili ya majilio.
Dominika
ya kwanza tuliweka bayana nini wajibu wako katika kipindi cha majilio. Ni kukaa tayari
kwa kulitafakati Neno la Mungu, kupokea sakramenti na kutenda yote yaliyo mema daima.
Tuliweka mbele yako watu wanne ambao katika matayarisho ya ujio wa Bwana wanahusika
moja kwa moja, nao ni Nabii Isaya, Yohane Mbatizaji, Mtakatifu Yosefu na Mama Bikira
Maria mama wa Mungu. Katika Dominika ya pili Neno linatualika KUONGOKA NA KUANZA MAISHA
MAPYA.
Katika somo la kwanza nabii Isaya anawaalika wana wa Israeli ambao bado
wako utumwani Babeli kuwa na utulivu kwa kuwa ukombozi wao unakaribia. Wameteseka
na kujuta na hivi Bwana amesikia kilio chao. Nabii Isaya anaimba wimbo akiwaambia
Waisraeli wakatengeneze njia ya Bwana, wakanyoshe mapito yake na wakasawazishe milima
na mabonde. Yote haya Nabii Isaya, anawataka wasawazishe mioyo yao ili Bwana apate
kuingia ndani mwao. Kwa hakika anawaambia yule ajaye ni mkuu ambaye kwake yeye utukufu
wa Bwana utafunuliwa. Wote wanaalikwa kutangaza habari hiyo njema ya furaha juu ya
milima na miji ya Israeli. Mafundisho haya ni kwa ajili yetu hivi leo tukayashike
na yatupe nguvu, ndiyo kujiandaa vema kumpokea Masiya, tukitangaza habari ya ukombozi
na furaha katika miji yetu na vijiji vyetu, ikibidi hata tukitokea milimani.
Mtakatifu
Petro katika somo la pili anakazia ujumbe wa maandalizi akisema, katika kusubiri jambo
la msingi si kujua siku wala saa bali kukaa tayari kama askari alindavyo mlango na
asubirivyo kupambazuke. Bwana hakawii kutimiza ahadi yake ya kuja lakini atakuja siku
ambayo hatujui. Pamoja na hili Bwana hapendi hata mmoja apotee bali apokee toba. Kumbe
majilio ni kipindi cha toba, ni kipindi cha msamaha kwa wakosefu, ni kipindi cha kupanda
mazao kwa ajili ya mavuno mazuri ndio ujio wa Masiya. Kumbe mwaliko wa Mtakatifu Petro
ni wa kweli yaani kutubu na kuongoka ili kujenga tabia ya utakatifu, mwaliko kwa wote.
Mwinjili
Marko anarudia ujumbe uleule wa Nabii Isaya, yaani anakazia matayarisho kina ya njia
ya Bwana. Anataka kila mmoja wetu aondoe milima na mabonde katika njia atakayopita
Bwana. Nabii Yohane Mbatizaji ni kielelezo cha maandalizi hayo anapowaalika watu wakaondoe
vichaka na manyasi yasiyohitajika katika barabara ambayo ni mapito ya Masiya. Kwa
hakika barabara hii ni maisha ya kiroho, ni moyo wako, ni maisha yako katika ujumla
wake. Ni lazima maisha yetu yawe ni maisha ya kumpendeza Mungu yaani bila maotea ya
magugu katika shamba la ngano.
Ujio wa Masiya unaambatana na kuunda taifa
jipya na hivi unadai kukazia utayari katika maisha ya toba, maisha ya kumpendeza Mungu
na watu, maisha ambayo huruhusu mishumaa tuliyotaja katika Dominika ya kwanza iendelee
kuwaka mpaka Bwana atakapokuja. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.