Taalimungu iguse imani na maisha ya Watu wa Mungu!
Taalimungu ya kina inapata chimbuko lake katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa,
katika Ibada ya kuabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwa namna ya pekee kwa kutafakari
Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Mafumbo ya Imani hayana budi kugusa akili, utashi
na maisha ya wale wote wanaojitaabisha kutafuta elimu juu ya Mwenyezi Mungu, daima
wakiomba msada wa neema ya Roho Mtakatifu, ili aweze kuimarisha utashi wa binadamu
katika kuyatafakari matendo ya Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Hii ni changamoto
ambayo imetolewa na Kardinali Gerhard Ludwig Mùller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa
la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Rais wa Tume ya Kitaalimungu Kimataifa, iliyoanza
mkutano wake wa Mwaka mjini Vatican tarehe Mosi, Desemba 2014.
Kardinali Mùller
anawataka wajumbe wa Tume hii kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema akili na utashi
wao, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa, kwani huu ni wito maalum kabisa wanaopaswa
kuutekeleza wakitambua kwamba, wana dhamana kubwa katika maisha na utume wa Kanisa.
Wanataalimungu wanatakiwa kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari
za tumaini lililo ndani yao, kama anavyosema Mtakatifu Petro.
Taalimungu inafanya
upembuzi yakinifu kwa kujikita katika imani, utulivu na ukweli katika imani; mambo
msingi yanayopania kujenga msingi wa ufunuo wa Mwenyezi Mungu, mmoja katika Fumbo
la Utatu Mtakatifu. Hili ni Fumbo la Mungu linalojidhihirisha kwa namna ya pekee katika
historia ya ukombozi na kilele chake ni Neno wa Mungu kufanyika mwili na hivyo kuweza
kueleweka hata katika akili ya binadamu.
Taalimungu haina budi kujikita katika
maisha ya waamini, akili na uhalisia wa maisha unaojidhihirisha katika maadhimisho
mbali mbali kwa lengo la kupata dira na mwelekeo wa shughuli za kichungaji. Taalimungu
anasema Kardinali Mùller haina budi kuwa ni kielelezo cha imani katika matendo na
maisha ya waamini, kama ambavyo Fumbo la Utatu Mtakatifu linavyodhihirisha umoja.
Huu ndio msingi wa Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya
Millenia ya tatu ya Ukristo.
Yesu Kristo ni mwanataalimungu wa kwanza hata
kabla ya Maandiko Matakatifu na anajionesha kwa wafuasi wake kuwa ni njia, ukweli
na uzima na kwamba, hakuna ukweli pasi na maisha na wala maisha pasi na ukweli. Kwa
njia ya Yesu Kristo, wanataalimungu wanaweza kuufahamu ukweli uliojisadaka na kuwa
ni sehemu ya maisha kwa wafuasi wake.
Tume ya kitaalimungu kimataifa inatekeleza
wajibu na utume wake kwa njia ya mshikamano wa kijumuiya na kidugu, kwa kuheshimiana,
kushirikiana na ugudu, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kweli sanjari na kuheshimu
Mafundisho ya Kanisa pamoja na kuwajibika barabara mbele ya Khalifa wa Mtakatifu Petro
aliyepewa dhamana ya kuliongoza Kanisa la Kristo.