Tuangalie kwa kifupi masomo yetu yatuambia nini leo: Katika somo la kwanza twaona
tangazo la ukombozi kwa Waisraeli na wito wa kurudi kutoka utumwani. Je nasi pia tuko
utumwani? Mungu yupo – tuutafute wokovu, maadam unapatikana. Katika somo la pili –
anayekesha mara nyingi aweza kuona siku zinakawia. Bali Bwana atupa sisi nafasi ya
kukiri dhambi, kutubu na kumwongokea.
Katika Injili – twaona kuwa ujio ya
Yesu Kristo unatayarishwa au kuonekana na Nabii muungamaji. Kwa mfano wake wa maisha
na Neno lake – mioyo ya watu imepata kuandaliwa kwa ujio wa Bwana. Yohane anawaita
watu watoke, waonekane katika uwazi, ili Mungu awapate. Waisraeli walikutana na Mungu
jangwani, waliacha yote, walikuwa watupu – Mungu akapata nafasi ya kuwaita.
Mhubiri
maarufu Munachi anaanza mahubiri yake jumapili hii ya leo akitoa mfano huu ; Mfano
wa mtoto na mgeni; Mgeni anaenda nyumbani kwake na kuuliza - Baba yupo? Jibu
la mtoto – ndiyo. Mgeni- naweza kuongea naye. Mtoto anajibu kwa sauti ndogo
kabisa - hapana.
Mgeni anaendelea - Mama yupo? Mtoto– ndiyo. Lakini pia
mtoto anaendelea kumjibu mgeni kuwa hawezi kuonana naye. Mgeni anaendelea – Je, yupo
mtu mwingine yeyote ninayeweza kuongea naye? Mtoto anajibu - ndiyo yupo Polisi.
Mgeni anataka kuongea naye? Mtoto anajibu hapana kwa vile anaongea na mzima
moto. Mgeni anauliza - ulizuka moto? Mtoto anajibu hapana ila wananitafuta. Hakika
katika mazingira kama haya yaonekana wazi kuwa mtoto huyu amejificha na anatafutwa
na wazazi wake. Asipotoka nje na kuonekana hakika hatapatikana. Ndicho kinachoonekana
leo katika masomo yetu na tafakari yetu ya leo. Mungu yupo amejionesha, anatutafuta
na anataka tukutane naye. Ila pengine mazingira yetu hayatoi nafasi ili kukutana naye.
Katika
Biblia - Jangwa laonesha sehemu iliyo wazi, panapoonekana. Haja ya kutoka nje ni muhimu,
ni lazima wahusika watoke nje ili waonekane. Leo Yohane Mbatizaji aliyeishi alichofundisha
anaenda Jangwani. Sote twaitwa tutoke ndani yetu tuende nje, tuende kukutana na Mungu.
Mwaliko wa kujuta na kuungama dhambi zetu huku tukimngojea huyo ajaye tukiwa tuko
tayari. Ni kipindi cha kutambua mahitaji yetu ya Mungu.
Kipindi cha majilio
ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini. Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa
Kanisa anasema, Mungu ametuumba sisi kwa ajili yake. Na ametuumba bila hiari yetu
ila kuupata wokovu ni juhudi binafsi. Na anaendelea kusema - mioyo yetu haitatulia
ila kwa Bwana. Hivyo wito wa kutoka ndani na kwenda nje uko wazi hapa. Yohane Mbatizaji
amefanya hilo na akawavuta watu. Kinachotakiwa hapa ni uongofu toka ndani - metanoia.
Mtakatifu Yohane atuita na anafanya jambo - yeye anaenda jangwani anafanya anachosema
na watu wanamfuata wanapata wanachohitaji.
Wito wetu leo tuwe mwanzo wa Injili,
yaani watangazaji wa habari njema. Tuangalie mahitaji yetu ya leo na mahitaji ya ulimwengu
wetu wa leo? Ili hiyo habari njema iseme zaidi miongoni mwa watu? Yesu ndiye kamisaa,
Yohane mbatizaji mwamuzi wa Mpira na sisi washika vibendera - tuko pamoja au tumeangalia
vitu vingine tu? Ubinafsi wetu tu?
Mwinjili Marko anaanza injili akitangaza
uwepo wa Mungu kati yetu - sisi tunaalikwa kuwa wajumbe wa uwepo wa Mungu hapa duniani.
Kipindi cha majilio kimewekwa ili tuweze kumwona tena Yesu kati yetu. Mfano wa mpiga
Zumari maarufu – Paganini -ni baada ya kupiga muziki kwa muda mrefu anagundua baadaye
sana kuwa mpiga muziki ni yeye na si kile chombo anachotumia. Muziki unatoka ndani
yake na si katika chombo. Chombo chatumika kama kifaa tuu. Hivyo nasi pia hatuna budi
kutambua haja ya kuwa wachezaji wa mchezo, watangazaji wa hiyo Habari Njema na si
kinyume chake.
Tumsifu Yesu Kristo. Imeandaliwa na Pd. Reginald Mrosso,
C.PP.S.