2014-12-03 14:37:11

Ilikuwa ni hija ya amani na majadiliano ya kiekumene!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Desemba, 2014, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko Xsaveri amefanya rejea katika hija yake ya kiekumene nchini Uturuki, kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Desemba, Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume.

Baba Mtakatifu amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka alizomkirimia wakati wa hija yake ya kiekumene nchini Uturuki. Anatumaini kwamba, majadiliano kiekumene kati ya Wakristo na yale ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam yataendelea kuboresha mahusiano na udugu kati ya waamini wa dini hizi. Uturuki ni nchi ambao ina utajiri mkubwa wa kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa. Maisha ya kiroho yana nafasi ya pekee sana nchini Uturuki, ambayo kimsingi ina waamini wengi wa dini ya Kiislam.

Baba Mtakatifu anasema, alipotembelea mjini Ankara, Uturuki, lengo lilikuwa ni kukazia umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru wa kidini kwa wote pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kujenga na kudumisha mshikamano, haki na amani. Akiwa Istanbul, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na waamini wa Kanisa Katoliki pamoja na viongozi kadhaa wa Jumuiya za Kikristo, kwa pamoja walimwomba Roho Mtakatifu, kuendelea kuliongoza na kulisaidia Kanisa kukua na kuimarika katika umoja na uaminifu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kilele cha hija yake ya kiekumene nchini Uturuki, kilikuwa ni hapo Jumapili tarehe 30 Desemba 2014, Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume, alipounganika na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kusali na hatimaye, kutia sahihi tamko la pamoja linalopania kuimarisha umoja wa Makanisa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea nia hii njema kwa Kanisa kutaka kutangaza Habari Njema ya Wokovu; kuheshimiana na kuendeleza majadiliano ya kidugu, ili kumwilisha ujumbe wa Kristo unaojikita katika ukweli, amani na upendo.

Baba Mtakatifu amewaambia mahujaji kwamba, Kipindi cha Majilio, kiwasaidie kujiandaa kwa ajili ya ujio wa Yesu Kristo Mfalme wa amani na kwamba, waendelee kusali ili hija yake ya kichungaji nchini Uturuki ilete umoja na mshikamano kati ya Wakristo sanjari na amani huko Mashariki ya Kati.

Majilio iwe ni fursa ya kushikamana na Yesu, kwa kuonesha mshikamano wa upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wasali ili kweli watu waweze kuishi kwa amani na utulivu, huku imani na mapendo vikimwilishwa sanjari na kuwatangazia Watu wa Mataifa kwamba, Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa umoja wa Kanisa; wamwombe ili asaidie kuonesha njia itakayowapeleka Wakristo katika umoja kamili, unaomwilishwa katika maisha ya kila siku. Waamini waendelee kuungana naye, ili kuwaombea Wakristo Mashariki ya Kati, waweze kuwa na imani thabiti, upendo na matumaini na kwamba, uwepo wao kiwe ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kuwasalimia wagonjwa waliokuwa wanafuatilia Katekesi yake kutoka kwenye Ukumbi wa Paulo VI ulioko mjini Vatican, kutokana na wasi wasi wa mvua kubwa kunyeesha. Amewasihi kusali kwa ajili yake.All the contents on this site are copyrighted ©.