2014-12-03 15:03:16

Hatua zilizokwisha kuchukuliwa dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia nchini Tanzania!


Ifuatayo ni risala ya mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia nchini Tanzania, katika kongamano lililofanyika Jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 3 Desemba 2014.

Kwanza nianze kwa kuwashukuru sana TGNP Mtandao na GTI kwa kunipa heshima hii ya kipekee ya kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka huu 2014. Sote tumesikia maelezo ya Kaimu Mkurugenzi juu ya historia na chimbuko la siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia, ambazo leo tunaadhimisha.hii ni fursa ya kipekee kwetu sote kutafakari kwa kina mazingira tunayoishi na jinsi ambavyo tunawajibu mkubwa wa kupambana na tatizo hili.

Pili niendelee kuwashukuru TGNP Mtandao na GTI kwa kazi nzuri ya kupambana na ukatili wa Kijinsia na kutoa elimu kwa Jamii ambayo wanaifanya kuanzia ngazi ya Jamii hadi taifa. Nimeelzwa kwamba tayari mmefanikiwa kufanya mafunzo kwa viongozi mbalimbali wa serikali za mitaa juu ya ukatili wa Kijinsia, Maahakimu wa Mahakama za mwanzo, Jeshi la polisi, watendaji wa halmashauri, wahudumu wa afya, na wanaharakati wa ngazi ya Jamii kupitia vituo vya taarifa na maarifa mikoa ya Mara, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, Dar e salaam na Pwani.

Nina uhakika kwamba mafunzo ya ukatili wa Kijinsia ambayo mmeyatoa kwa viongozi hawa yataleta mabadiliko chanya muda sii mrefu kwababu tutakapokuwa na viongozi au watendaji wenye uelewa wa masuala haya ni dhahiri kwamba watayashughulikia matukio ya Ukatili wa Kijinsia kwa umakini na weledi zaidi. Tunaamini viongozi hawa ni hazina kwa miaka ijayo na tatizo hili litapungua au kuisha kabisa.

Nimefurahi pia kusikia kwamba TGNP Mtandao kupitia GTI, hivi karibuni mliwakutanisha viongozi wa dini, mila, Jamii na wanasiasa pamoja kutoka katika ngazi ya wilaya na kuwajengea uwezo juu ya masuala ya haki za Binadamu na Ukatili wa Kijinsia. Elimu hii haitapita bure ni mkakati mzuri ambao utaleta mabadiliko chanya muda sii mrefu. Sisi Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora tunawatia moyo muendelee na jitihadi hizi ili kuleta mabadiliko katika Jamii yetu, kwani serikali peke yake haiwezi kufika kila mahali na kutoa elimu. Na tunaamini kwamba hii ndio njia pekee ya kuleta mabadiliko kwa kukutana wadau mbalimbali na kuzungumza nao.

Ndugu zangu wanaharakati, tunapotumia siku ya leo kutafakari juu ya namna ya kukomesha kabisa ukatili wa Kijinsia hususani kwa wanawake tunajukumu la kuangalia mazingira tunayaoyaishi kama yanatuwezesha kufanikisha vita hiyo. Kila mmoja analojukumu kubwa, vyombo vya umma/dola, taasisi za umma, watu binafsi, mitandao na wanaharkati wanajukumu kubwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia, huwezi kuleta maendeleo kama watu wanteseka, kwahiyo kila kundi lina jukumu la kupambana na ukatili wa kijinsia.

Vita dhidi ya Ukatili wa Kijinsia inahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa wanaanchi na viongozi ngazi zote ili ikomeshwe. Vita dhidi ya ukatili wa kijinsia haina mwanamke wala mwanamume, ni lazima tupate watu wa kutosha kutoka jinsi zote watakaouangana kudai mabadiliko. Wanaume mlioko hapa ninyi ni wadau muhimu sana katika kuleta mabadiliko chanya ya kukomesha kabisa ukatili wa kijinsia.

Ushiriki wenu katika mapambano haya ni mafanikio makubwa kwasababu sote tunatakiwa kukataa vitendo vya kikatili kwa binadamu na hasa Mwanamke na makundi yaliyoko pembezoni kama walemavu nk.

Ndugu zangu wanaharakati, pamoja na kwamba sio wanaume wote wanasababisha ukatili wa kijinsia, lakini ili kufanikisha mapambano haya wanaume wana jukumu kubwa, kwanza kuwaelimisha wanaume wenzao, pili kuwafikia watu wengi zaidi kutokana na kwamba wao wanafursa zaidi ya kutembea kuliko wanawake ambao wakati mwigine mzigo wa kazi za kifamilia umewaelemea hasa kulea watoto.

Ndugu zangu wanaharakati, hivi sasa Tanzania inatajwa kuwa ni moja ya nchi zilizokidhiri kwa tatizo la mimba za utotoni. Katika ripoti ya UNFPA ya mwaka 2013 imeitaja Tanzania kama nchi inayoinakabiliwa na ongezeko kubwa la mimba za utotoni na hivyo kuwafanya wasichana wengi kukatiza ndoto yao ya kimaisha. Sisi tunasikitika kwamba hali hii bado inaendelea licha ya jitihada za serikali na wadau wengine kama TGNP Mtandao zinzoendelea huko vijijini kutoa elimu kwa jamii. Ni lazima sote tutambue kwamba ukimpa mtoto wa kike mimba ambaye hajamaliza masomo ni kosa la jinai, na kwa mujibu wa sheria ya makosa maalum ya kijiamiana (SOSPA) 2008 ni kosa la jinai na ni ubakaji.

Ngugu zangu wanaharakati! niwaeleze ukweli, hakuna mazungumzo kwenye hili anayefanya ukatili wa kijinsia ni lazima achukuliwe hatua stahiki na wazazi msiendekeze hili, toeni taarifa kwa vyombo vya dola kwa kushirikiana na walimu wakuu wa shule anaposoma mtoto, sheria itachukua mkondo wake.

Vyombo vya dola vionapaswa kuchukulia kwa umakini kesi za ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua stahiki. Kesi ya Ukatili wa Kijinsia isshie polisi, au kwenye dawati la Jinsia na watoto, ipelekwe mahakamani ili muhusika achukuliwe hatua za kisheria. Matukio yameongezeka kwa kasi kutokana na kesi nyingi kumaliziwa nje ya mahakama, wito wetu kwa jamii tuungane kuvisaidia vyombo vya dola kuwashtaki wanaobaka, kulawiti, kupiga au kujeruhi wanawake, wanaowapa watoto wa shule mimba na wanaoshiriki vitendo vya ukeketaji. Wananchi wanaweza kukomesha kama wataamua kuripoti na kukataa kuhongwa na watuhumiwa kwa kigezo cha kurudisha kesi nyumbani.

Ninawataka wazazi msikubali kuwa mawakala wa ndoa za utotoni. Msikubali kuzungumza na wabakaji au wanaowatia watoto mimba nje ya mahakama, mtu akishafanya kosa akafikishwa mbele ya sheria viachinei vyombo hivyo vifanye kazi yake, sheria zipo na zitatumika.

Ndugu zangu wanaharakati, Kwanza ni lazima tutambue kwamba ukeketaji ni kosa, sheria zetu haziruhusu, kama vile tunavyopiga vita vitendo vya kushambuliwa au kuuawa kwa watu wanaoishi na ulemevu wa ngozi(Alibino) au wanawake wazee.
Ni lazima kila mmoja wetu aheshimu haki za msingi za kuishi, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) ibara ya 14 na 15 zimeeleza wazi.

Sisi tunataka kila mwanadamu aheshimu utu na ubinadamu wa mwezake, wanawake wa vijijini ambo macho yao yamekuwa mengundu kwasabau ya matumizi ya kuni au maradhi wanapaswa kuheshimiwa kama binadamu wengine na kulindwa uhai wao. Wanaofanya vitendo vya kuwashambulia ni lazima watajwe na wachukuliwe hatua.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI KATIKA KUKABILIANA NA HALI HII
Ndugu zangu wanaharakati; Kutokana na hali inavyokweda serikali imeweka mikakati mikubwa na hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni kurekebisha sheria kandamizi na kutunga sheria mpya zinazozingatiwa usawa wa kijinsia na haki za binadamu.

Kuwepo kwa sheria kandamizi kumewafanya wanawake kutopata haki zao kikamilifu. Pamoja na kuwa Katiba ya Tanzania imeainisha kuwepo kwa haki sawa kati ya wanawake na wanaume, bado usawa huo haujafikiwa. Katika kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao, baadhi ya sheria zimetungwa na zingine kufanyiwa marekebisho ambazo ni:

· Sheria ya Makosa ya Kujamiiana yaani The Sexual Offences (Special Provisions) Act (SOSPA) ya 1998, ambayo imefanyiwa marekebisho na kuhuishwa kwenye ‘Penal Code”. Sheria za Ardhi za Mwaka 1999( yaani The Land Act 1999 na Village Land Act 1999) katika sheria hizi mbili Serikali iliendelea kufanya marekebisho na ambapo mwaka wa 2004 ilifanyia marekebisho sheria ya utatuzi wa migogoro ya Ardhi (Land Dispute settlement Act, 2004) ambapo pamoja na mambo mengine uwakilishi wa wanawake katika Mabaraza yanayoamua masuala ya ardhi uliwekwa kisheria ili Mabaraza hayo yawe na sura na uwakilishi kamili wa Kijinsia.

· Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini na 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika ajira na likizo ya Uzazi. · Sheria ya Utumishi ya Mwaka 2002, ambayo ilidurusiwa mwaka 2007, nayo imetoa fursa sawa za ajira Serikalini kwa wanawake na wanaume na imetoa upendeleo kwa wanawake katika ajira. · Sheria ya Kuzuia usafirishaji wa binadamu. (Anti-traffiching Act, 2007) · Sheria ya UKIMWI, (2008) · Sheria Mpya ya Mtoto (The Law of the Child Act, 2009) ambayo tayari imeshapitishwa na Bunge imelenga katika kumpunguzia mwanamke mzigo wa matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa.

Ndugu zangu wanaharakati; Tunaendelea kushirikiana na serikali ili katika mchakato huu wa katiba mpya masuala muhimu ya haki za wanawake yaweze kusimamiwa na kutokuondolewa, kuhakikisha kwamba inatoa mweleko wa kuwalinda wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni dhisi ya ukatili wa Kijinsia. Niwashukuru sana kwa kujitokeza katika kampieni hii ili sote tuweze kuunganihsa nguvu na kupambana na ukatili wa Kijinsia. Ninawashukuru tena TGNP Mtandao na mashirika mengine mlioshirikiana katika kuandaa siku hii, kwa kunipa heshima hii na kunialika katika kuendeleza kampeni hii ili mwisho tushinde.
Ninawashukuru na ahsanteni kwa kunisikiliza


HALI HALISI YA UKATILI WA KIJINSIA HAPA NCHINI TANZANIA

Ukatili wa Kijinsia ni mojawapo ya matatizo yanayoikabili Tanzania. Taarifa ya ‘Tanzania Demographic and Health Survey’ ya mwaka 2010 imebainisha kuhusu takwimu za ukatili wa kijinsia kama ifuatavyo:-
· 1/3 ya wanawake walio na umri kati ya miaka 15-49, wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na wenzi wao au ndugu zao.
· Wanawake 2 kati ya 5 wamefanyiwa ukatili tangu wakiwa na miaka 15
· Asilimia 44 ya wanawake walio katika ndoa wenye umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili na waume au wapenzi wao.
· Asilimia 20 ya wanawake walio na umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kingono na wapenzi wao au wapenzi wao wa zamani. Aidha, mwanamke mmoja kati ya 10 walilazimishwa kufanya mapenzi kwa mara ya kwanza.
· Kuhusu tatizo la ukeketaji, utafiti unaonyesha kuwa limepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2005 hadi 15 mwaka 2010. Aidha, t akwimu hizo zinaonyesha kuwa asilimia 15 ya wanawake wamekeketwa. Mikoa inayoongoza katika ukeketaji ni Manyara,(71%), Dodoma, (64%), Arusha, (59%), Singida,(51%) Mara (40%), Morogoro, (21%) na Tanga ( 20%).

Mwaka 2013 (Takwimu za Wizara ya afya)
Wakazi wa vijijini
73.3%
Wakazi wa mijini
26.7%
Idadi ya watu chini ya umri wa miaka 24
65%

Ukosefu wa ajira kwa vijana

Vifo vya uzazi
454 kwa kila vizazi hai 100,000
Mimba za utotoni
23% ya wasichana wenye umri kati ya 15-19 walikuwa mimba au wana watoto
Ndoa za Utotoni
18% ya wasichana wa umri kati ya miaka 15-19
Wanawake waliokeketwa
15%

Ukosefu wa ajira kwa vijana wa umri kati ya 15 – 24 ilikuwa 13.4% mwaka 2012. Kwa wanawake ni (14.3%) zaidi ya wanaume wa umri huohuo (12.3%).
Dawati la Jinsia na Watoto kwenye vituo vya polisi hapa nchini mwaka 2014.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2014 idadi ya ya ukatili wa kijinsia kwa watoto kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 519 hii ni pamoja na mikoa mitatu ya kipolisi yani Kinondoni, Temeke na Ilala, ikifuatiwa na Zanzibar 219 (Unguja Magharibi na kusini), Shinyanga 69, Mara 62, Tabora 55, Morogoro 36, Kagera 32 na mkoa wa Pwani 20


· ASILIMIA 35% ya wanawake duniani wanafanyiwa ukatili wa kimapenzi na wapenzi wao au watu wasiokuwa wapenzi wao
· Kwa wastani asilimia 30% ya wanawake ambao wameshawahi kuwa kwenye mahusiano walishawahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au wa kingono/kimapenzi
· Asilimia 38% ya mauaji ya wanawake duniani hufanywa na wapenzi wao/watu wenye mahusiano naoUKARIBISHO NA NENO LA UFUNGUZI SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA-TGNP Mtandao 03.12.2014

TGNP Mtandao na Chuo chetu cha Mafunzo GTI tunapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote katika ngongamano hili la wazi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia. Kama tunavyofahamu siku hizi huadhimishwa kimataifa kuanzia tarehe 25/11 hadi tarehe 10/12 kila mwaka. Ndani ya siku hizi 16 kuna matukio kadhaa ambayo yote yanahusu kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Tarehe 25/11 ni siku ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, 29/11 ni siku ya watetezi wa haki za wanawake , 1/12 ni siku ya ukimwi duniani, 3/12 siku ya watu wanaoishi na ulemavu duniani, 6/12 kumbukumbu ya mauaji ya kikatili ya wanawake 14 wa Motreal na 10/12 ni siku ya haki za binadamu duniani.

Lengo kuu la siku hizi 16 ni kuendeleza mijadala, kutafakari kwa pamoja kuhusu mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, mafanikio yake, changamoto na namna ya kujipanga na kusonga mbele kwa pamoja. Kila mwaka kunakuwa na kauli mbiu na kauli mbiu ya mwaka huu hapa Tanzania ni “Funguka! Fichua Ukatili kwa afya ya jamii” Hii ina maana kuwa tuvunje ukimya kila tunaposhuhudia kitendo chochote cha ukatili wa kijinsia tuchukue hatua. Aidha kauli mbiu itayoongoza mjadala wetu wa leo ni “Siyumbishi, Najilinda Mnilinde” kauli mbiu hii inalenga vijana kwani tunaamini kuwa mapambano haya yanahitaji nguvu kubwa na ya pamoja. Vijana ni zaidi ya 60% ya watanzania wote. Hii ni idadi kubwa sana.

Tunatarajia hawa vijana ndio watakaoendesha taifa hili kwa miaka hamsini ijayo hivyo basi mikakati yetu lazima iwalenge vijana. Vijana hususan vijana wa kike wanakabiliwa pia na ukatili wa kijinsia kwa kiasi kikubwa. Hivyo basi wanatakiwa kujilinda dhidi ya mazingira hararishi ambayo yanaweza kuwasababishia kukumbana na ukatili wa kijinsia. Jamii pia inajukumu kubwa la la kuwalinda vijana katika kuwatayarishia mazingira bora dhidi ya ukatili wa kijinsia kuanzia nyumbani, shuleni vyuni hadi maofisini.

Tatizo la jira ni kubwa sana na kwa kiasi kikubwa linasababisha ukatili kwa wasichana hususan ule wa ajira zisizo na utu, usafirishaji haramu wa wasichana, biashara ya ngono, rushwa ya ngono , ndoa za utotoni n.k. Tunasisitiza uwepo wa mabweni ya kutosha katika shule zote za sekondari za kata na nyigine hususan ya wasichana ili kupunguza umbali na mazingira hatarishi kwenda shuleni.

Ndugu mgeni rasmi, tunatarajia kuwa baada ya mjadala huu vuijana wetu watakuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia na kuitekeleza kauli mbiu hii ya kutokuyumbisha, kujilinda na jamii kuwalinda.

Ndugu mgeni rasmi, TGNP kwa kushirikina na wadau wengine tunaungana na wenzetu kote duniani kupinga ukatili wa kijinsia. Mapambano haya yameanza muda mrefu japokuwa hali bado si nzuri kwani takwimu zinaonesha kwamba 1/3 ya wanawake waliona umri kati ya miaka 15 –49 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na wenzi au ndugu zao. Wanawake 2 kati ya 5 wamefanyiwa ukatili tangu wakiwa na miaka 15. Asilimia 44 ya wanawake walio katika ndoa kati ya umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili na wenzi wao. 20% ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kingono na wapenzi wao.

Takwimu za wizara ya afya zinaonesha, katika mwaka 2013 asilimia 23% ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 19 walikuwa na mimba au walikuwa na watoto huku zikionesha kuwa asilimia 18% ya wasichana wa umri huo huolewa utotoni. Wasichana 4 kati ya 10 ni wahanga wa mimba za utotoni. Mwaka 2012 wasichana 8000 waliacha shule kutokana na mimba za utotoni na kati ya hao 3000 walikuwa shule za msingi. Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa bado ukeketaji ni tatizo kubwa likiwa bado linatendeka kwa asilimia 15%. Pia asilimia 14.6 ya wanawake wa Tanzania wamefanyiwa ukeketaji. Mikoa inayoongoza kwa ukeketaji ni manyara 70.8%, Arusha 58.6% na Mara 39.0% ( 2010).Hali hii inatisha na inahitaji nguvu ya ziada ili kukomesha ukatili huu.

Ndugu mgeni rasmi, Serikali yetu imejitahidi kwa kiasi kupambana na tatizo hili. Utashi wa kiasiasa upo kwani Serikali imeridhia mikataba na matamko mengi kuhusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia mfano mkataba wa kutokomeza aina zote za ukatili na dhuluma dhidi ya wanawake na watoto (CEDAW); Mkataba wa nyongeza wa Maputo (Maputo protocol), Mkataba wa SADC wa usawa wa Jinsia ( SADC Gender Protocol) pamoja na Mkataba wa haki za watoto ( CRC), Tamko la Kimataifa la haki za binadamu ambalo linatambua haki za wanawake na watoto kama mojawapo ya haki za binadamu. Hapa nchini pia serikali imetambua na kubaini kwa mara ya kwanza msingi wa usawa wa kijinsia na haki za wanawake katiba pendekezwa, pia dira ya Taifa ya 2025 imebainisha pia usawa wa kijinsia kama msingi wa maendeleo endelevu.

Usawa wa Kijinsia ni katika Nyanja zote za uongozi kwasababu wanawake ndio waadhirika wakubwa na wasipokuwa kwenye nafasi za uongozi ni tatizo. Ndio maana TGNP Mtandao na wadau wengine tumekuwa tukidai uwakilishi 50/50 kwenye nafasi za maamuzi. Uchaguzi Mkuu na huu wa serikali za mitaa utakaofanyika Disemba 14, ni fursa ya pekee ya kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanaingia kwenye uongozi.

Tumeshuhudia pia Chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto uanzishwaji wa madawaji ya jinsia katika vituo vya polisi, Madawati ya jinsia katika wizara zote pamoja na mwongozo wa kupambana na ukatili chini ya wizara ya Afya. Pamoja na hayo yote bado tatizo ni kubwa.
TGNP Mtandao na GTI tumejitahidi kupambana na ukatili wa Kijinsia kwa kutoa elimu kwa Jamii katika ngazi zote, kufanya mafunzo mbali mbali kwa wadau mbali mbali mfano; Jeshi la polisi yakiwemo madawati ya jinsia, viongozi wa Dini, Viongozi wa Mila, Mahakama, viongozi mbalimbali wa serikali za mitaa, , watendaji wa halmashauri, wahudumu wa afya, na wanaharakati wa ngazi ya Jamii kupitia vituo vya taarifa na maarifa mikoa ya Mara, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, Dar e salaam na Pwani.

Ndugu mgeni rasmi, ni juzi tu tumehitimisha tumewakutanisha viongozi wa dini, mila, Jamii na wanasiasa pamoja kutoka katika ngazi ya wilaya na kuwajengea uwezo juu ya masuala ya haki za Binadamu na Ukatili wa Kijinsia. Tunaamini kuwa tatizo ni kubwa na linahitaji nguvu za pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali. Na hivi tunavyoongea kuna wenzetu wako Tarime kuwanusuru vijana wa kiume dhidi ya tahara za kimila ambazo zinasababisha maumivu makali, kuvuja damu hadi kufa pamoja na kupata athari nyingine za kiafya. Zaidi ya Wavulana 150 watakuwa katika kambi huko SIRARI Tarime wakipata elimu ya ujinsia na stadi za maisha pamoja na tohara salama. Mangariba 15 nao pia wanapatiwa mafunzo ya ujasiria mali na stadi za maisha ili waweze kujitambua pia kujipatia kipato mbadala badala ya kutegemea ukeketaji kama njia ya kupata kipato. Nipende kushukuru sana UNFPA kwa kuwa pamoja nasi katika vita hii.

Ndugu Mgeni rasmi, Vita dhidi ya Ukatili wa Kijinsia inahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa wanaanchi na viongozi ngazi zote ili ikomeshwe. Vita dhidi ya ukatili wa kijinsia haina mwanamke wala mwanamume, ni lazima tupate watu wa kutosha kutoka jinsi zote watakaouangana kudai mabadiliko. Wanaume mlioko hapa ninyi ni wadau muhimu sana katika kuleta mabadiliko chanya ya kukomesha kabisa ukatili wa kijinsia.

Ushiriki wenu katika mapambano haya ni mafanikio makubwa kwasababu sote tunatakiwa kukataa vitendo vya kikatili kwa binadamu na hasa Mwanamke na makundi yaliyoko pembezoni kama walemavu nk.

Pia tunapenda kukumbusha kila mmoja wetu kuhusu wajibu wetu katika hii vita dhidi ya ukatili wa kijinsia. Kula mmoja wetu ajilinde dhidi ya ukatili wa kijinsia, Jamii tuwalinde vijana na watoto na kila mtu dhidi ya ukatili kwa kuweka mazingira salama. Kwa serikali bado suala la rasilimali hususam bajeti ni changamoto kubwa. Rasilimali zinazotengwa haziendani na ukubwa wa tatizo. Ukitembelea madawati ya Jinsia utakubaliana na mimi. Tunatoa wito kwa Serikali kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya kupambana na tatizo hili la ukatili wa kijinsia.

Kipekee niwashukuru UNFPA na ACT kwa kuwezesha shughuli hii na washiriki wote kwa kujumuika nasi hii inaonesha nia ya dhati ya kupambana na ukatili wa kijinsia. Natumaini tutatoka na mkakati wa pamoja wa kuendelea na mapambano haya.
All the contents on this site are copyrighted ©.