2014-12-03 09:37:12

Australia itaendelea kushirikiana na Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!


Askofu mkuu Dominique Mamberti aliyekuwa Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, amehitimisha safari ya kikazi nchini Australia kama kilele cha maadhimisho ya Karne moja tangu nchi hii ilipopandishwa hadhi na kuwa ni sehemu ya utume wa Kanisa na miaka arobaini ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Australia na Vatican.

Akiwa nchini Australia, Askofu mkuu Mamberti amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na Serikali pamoja na kushirikishana mambo msingi yaliyojiri wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa G20 uliofanyika hivi karibuni nchini Australia. Wameshirikisha yale yanayoendelea huko Mashariki ya Kati: mchango wa Kanisa Katoliki na majadiliano yanayoendelea huko katika mchakato wa kutafuta haki, amani na utulivu.

Wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, Askofu mkuu Mamberti pamoja na wenyeji wake wamejadiliana kwa kina na mapana dhamana na utume wa familia. Wamekazia umuhimu wa watu kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya jamii inayowazunguka.

Akiwa nchini Australia, Askofu mkuu Mamberti amepata nafasi ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kutoa Sakramenti ya Kipaimara, kwa kuwataka vijana kuwa ni mashahidi wa Yesu Kristo na Kanisa lake ndani ya familia na sehemu mbali mbali za maisha yao. Ametembelea na kusali kwenye kaburi la Mtakatifu Mary MacKillop, mwamini wa kwanza kutoka Australia kutangazwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuwa Mtakatifu. Amepewa pia shahada ya heshima katika masuala ya kidiplomasia, tukio lililomwezesha kupembua kwa kina na mapana kuhusu mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya watu kwa kuwashukuru wote waliochangia kwa hali na mali.

Askofu mkuu Dominique Mamberti akizungumza na Maaskofu wa Australia, amejikita katika utume na dhamana inayotekelezwa na wanadiplomasia wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia; hali tete huko Mashariki ya Kati na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Australia, Jumapili tarehe 7 Desemba 2014 wataadhimisha Siku ya Mshikamano na Wakristo Mashariki ya Kati na kwamba, ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Australia utatembelea Iraq na Lebanon ili kuwatia shime Wakristo huko Mashariki ya Kati.

Askofu mkuu Mamberti alipata fursa ya kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Australia kwa kujikita zaidi katika vitendo vya kigaidi na mambo ambayo yanapelekea vijana wengi kujiunga na vitendo hivi vya kigaidi kiasi cha kutoogopa kufa; shida na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati; Majadiliano ya kidini na kiekumene nchini Australia; nyanyaso za wanawake na wasichana sehemu mbali mbali za dunia pamoja na mchango wa Serikali ya Australia kwa kushirikiana na Caritas Australia.

Askofu mkuu Mamberti ametembelea Makumbusho ya Kale na Kumbu kumbu za Vita kuu ya Pili ya Dunia, kwa kuangalia picha za watu waliojisadaka kwa ajili ya nchi yao. Ameadhimisha pia Siku kuu ya Papa kwa kumshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, anatarajiwa kuanza utume waka rasmi, mwezi Januari, 2015. Vatican itaendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Askofu mkuu Dominique Mamberti, kabla ya kurejea mjini Roma, ametembelea Chuo kikuu cha Kikatoliki nchini Australia, kwa kuwataka wadau kuhakikisha kwamba, wanasaidia kukoleza mchakato wa majiundo makini ya wanafunzi: kiroho, kimwili, kimaadili, kiutu na kitaaluma. Australia na Vatican katika kipindi cha miaka arobaini wameimarisha uhusiano wao wa kidiplomasia, kwa ajili ya mafao ya pande hizi mbili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.