2014-12-02 08:25:54

Watawa mnachangamotishwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka kuhusu Fumbo la Kanisa, Yaani "Lumen gentium", Mwanga wa Mataifa, wanawahamasisha watawa popote pale walipo kulidhihirisha Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yanayojikita katika tafakari ya Neno la Mungu, Sala na Matendo ya huruma, kama kielelezo hai cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Kwa njia ya uaminifu na udumifu katika wito na maisha yao ya kitawa, wanaendelea kumpamba Bibiarusi wa Kristo, yaani Kanisa kwa kuwahudumia watu kwa njia ya majitoleo na moyo mkuu. RealAudioMP3

Watawa watambue kwamba, changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha inapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mwaka wa Watawa Duniani uliozinduliwa katika Maadhimisho ya Jumapili ya kwanza ya kipindi cha Majilio, ili ni fursa kwa watawa sehemu mbali mbali za dunia kuupamba ulimwengu kwa njia ya harufu ya utakatifu wao unaojidhihirisha katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja maisha ya kijumuiya yanayofumbata umoja, udugu na mshikamano wa dhati.

Askofu mkuu Josephat Lpuis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani anasema kwamba, watawa wanapaswa kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Miito mbali mbali ya watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume inapata asili na utimilifu wake ndani ya Kanisa.

Hii ni changamoto kwa watawa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia bila ya kuingia katika kishawishi cha kujitafuta wenyewe, kwa kujiweka pembeni mwa mikakati ya shughuli za kichungaji inayotolewa na Makanisa mahalia.

Askofu mkuu Lebulu anawataka watawa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kushikamana na Familia ya Mungu katika ujumla wake, ili yote yafanyike kwa sifa na utukufu wa Mungu na mwanadamu aweze kukombolewa na kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa wanayo nafasi na wajibu mkubwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia, kumbe, watawa hawapaswi kujisikia kuwa ni wageni katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji kwani wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Lebulu anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, iwe ni fursa ya kutafakari na kumwilisha mashauri ya Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watawa; kwa kujikita katika Ufukara wa Kiinjili kwa njia ya maneno lakini zaidi kwa ushuhuda wa matendo yao; Utii wa Kiinjili unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kukazia Usafi kamili, kielelezo cha sadaka na majitoleo makubwa kwa ajili ya Mungu na jirani. Watawa washiriki kikamilifu katika maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ili waweze kuwasaidia waamini kulitafakari vyema Neno la Mungu na kulitolea ushuhuda kwa njia ya imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.