2014-12-02 15:23:19

Viongozi wa kidini wameamua kujifunga kibwebwe kupambana na utumwa mamboleo duniani!


Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya viongozi wakuu wa dini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ambao siku ya Jumatatu tarehe 2 Desemba 2014 wametia sahihi kwenye Tamko la pamoja la kupambana na utumwa mamboleo unaojionesha kwa namna ya pekee katika biashara haramu ya binadamu, kazi za suluba, ukahaba, biashara haramu za viungo vya binadamu pamoja na mambo yote ambayo yanashindwa kuheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu hayana budi kutamkwa kwamba ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Viongozi wa kidini wameamua kulivalia njuga tatizo hili kwa kuwasaidia watu kwa mawazo na matendo, ili kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, waweze kukomesha utumwa mamboleo, kwani kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ana haki ya kupewa heshima na udugu. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna uwezekano mkubwa wa kufuta kabisa utumwa mamboleo kutoka katika uso wa dunia na kwamba, huu ni wajibu wa viongozi wa dini kimaadili.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa viongozi wa kidini pamoja na umati mkubwa wa watu uliokuwa umekusanyika mjini Roma kushuhudia tukio hili la kihistoria anasema kwamba, utumwa mamboleo unaendelea kunyanyasa na kudhulumu, utu na heshima ya binadamu, changamoto kwa viongozi wa kidini kushirikiana katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo. Hawa ni watu wanaonyanyasika: kimwili, kiuchumi, kingono na kisaikolojia.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mungu ni upendo na chimbuko la uhuru kamili, unaofungamanisha mahusiano ya kijamii, kwa ajili ya mafao ya wengine katika hali ya usawa na udugu. Watu wote ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na wanapaswa kutambulikana kutokana na utu wao. Viongozi wa kidini anasema Baba Mtakatifu wameamua kujifunga kibwebwe ili kupambana na mfumo mzima wa utumwa mamboleo, unaowaathiri zaidi maskini, kiasi cha kuuzwa kama bidhaa.

Wanyonge hawa ndio wanaopaswa kulindwa na kutetewa dhidi ya biashara haramu ya binadamu, ngono na viungo; matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kazi za suluba wanazofanyishwa watoto, kiasi cha kuathiri malezi na makuzi yao. Utumwa huu unafanyika kila sehemu ya maisha ya mwanadamu na kwamba, tatizo hili linazidi kukua na kuongezeka mwaka hadi mwaka, changamoto kwa viongozi na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati dhidi ya utumwa mamboleo, kwa kufanya kwanza toba na wongofu wa ndani, ili kila mtu aweze kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.