Professa Mussa Juma Assad achukua mikoba ya Bwana Ludovick Utouh nchini Tanzania!
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Taarifa iliyotolewa Jumatatu, Desemba
Mosi, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema kuwa uteuzi wa Bwana
Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu, 2014. Taarifa hiyo imeongeza kuwa Bwana Assad
ameapishwa Jumanne, Desemba 2, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Kabla
ya uteuzi wake, Bwana Assad alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Bwana Ludovick Utouh ambaye amestaafu kwa
mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma. Profesa Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi
na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana Shahada ya Uzamivu wa
Uhasibu (PHD in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001
na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti wa Fedha (MA in Financial Accounting) kutoka
Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.
Profesa Assad pia
ana Stashahada ya Kitaaluma ya Uhasibu (Professional Diploma in Accounting) kutoka
Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na Shahada ya Biashara (Bachelor of Commerce)
ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1988. Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa
Assad anao uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi. Alikuwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 - 2014); ni Rais na Mjumbe
wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012;
na ni mjumbe wa Bodi kadhaa za Wakurugenzi nchini Tanzania.
Katika kumteua
Profesa Mussa Juma ASSAD kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Rais
Kikwete anayo imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu ambao Profesa Assad
anao utamwezesha kutekeleza vema majukumu ya nafasi hiyo muhimu sana katika utawala
bora wa Tanzania.