2014-12-02 08:01:38

Mwaka wa Maskini Jimbo kuu la Manila!


Jimbo kuu la Manila, nchini Ufilippini, kwa maadhimisho ya Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, limezindua rasmi Mwaka wa Maskini, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 500 ya uwepo wa Ukristo nchini Ufilippini, Jubilee ambayo itafikia kilele chake kunako mwaka 2021. RealAudioMP3

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kufikiri na kutenda kwa ajili ya kuonesha mshikamano wa dhati na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini wa hali na kipato!

Waamini wanakumbushwa kwamba, Yesu mwenyewe alionesha moyo wa ufukara katika Fumbo la Umwilisho, katika yote akawa sawa na binadamu, lakini hakuwa na dhambi; alionesha huruma na upendo kwa maskini na wagonjwa wa nyakati zake, kwa kuwaponya na kuwaondolea dhambi zao. Kuna maelfu ya watu nchini Ufilippini yanayoogelea kwenye dimbwi la umaskini wa hali na kipato, mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Umaskini mkubwa unachangiwa pia na majanga asilia ambayo yamekuwa ni chanzo kikuu cha mateso na mahangaiko ya wananchi wengi wa Ufilippini, bila kusahau rushwa na ufisadi wa fedha na mali ya umma. Mapambano dhidi ya umaskini ni mchakato pevu unaohitaji mshikamano na wafdau mbali mbali, kila kundi likijitahidi kutekeleza dhamana yake kikamilifu.

“Simama na tembea!” Ndiyo kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Mwaka wa Maskini nchini Ufilippini, kwani Kanisa kwa upande wake, halina dhahabu wala fedha, bali imani na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mambo ambayo yakitumiwa kwa njia ya upendo unaojikita katika mshikamano wa dhati, baa la umaskini linaweza kupewa kisogo nchini Ufilippini, ingawa haya ni mapambano pevu.

Ni matumaini ya Jimbo kuu la Manila kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Maskini, yataweza kuwashirikisha na kuwagusa watu wengi zaidi kutambua kero na adha ya umaskini miongoni mwa jamii.

Watu wakumbuke kwamba, siku ile ya mwisho watahukumiwa kwa jinsi ambavyo wameweza kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kumwilisha upendo wa Mungu kwa maskini na wote wanaohitaji msaada, kama kielelezo makini cha kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.