Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu Barani Ulaya!
Amini, usiamini lakini takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu laki nane ambao
wametumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu katika nchi za Jumuiya ya Ulaya,
jambo ambalo linadhalilisha utu na heshima ya watu hawa, ambao wengi wao ni wale wanaotoka
katika mazingira hatarishi zaidi.
Haya yamebainishwa hivi karibuni na Tume
ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kwenye Jumuiya ya Ulaya, COMECE wakati
wa majadiliano yaliyokuwa yanaongozwa na kauli mbiu "Kanisa na Jamii yaliyofanyika
mjini Brussels, Ubelgiji.
COMECE katika taarifa yake baada ya majadiliano haya
inaonesha kwamba, asilimia 60 ya waathirika wa biashara haramu ya binadamu wanatoka
katika nchi zinazounda Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, changamoto ya kukuza na kuendeleza
ushirikiano kati ya Serikali, vyama vya kiraia na Kanisa ambalo limekuwa mstari wa
mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu ambayo ni kielelezo cha
mwendelezo wa utumwa mamboleo na uhalifu wa kimataifa. Biashara hii haramu inaendelea
kushamiri sehemu mbali mbali za dunia kiasi cha kushika nafasi ya tatu kimataifa baada
ya biashara haramu ya dawa za kulevya na silaha duniani.
Watu wanaotumbukizwa
kwenye biashara haramu ya binadamu; wanawake, wasichana na watoto wanafanyishwa biashara
ya ukahaba; baadhi yao wanafanyishwa kazi za suluba kwa kulipwa "kiduchu"; baadhi
ya wanawake wanabebeshwa mimba za chupa pamoja kuasi watoto kinyume cha sheria. Takwimu
zinaonesha kwamba, asimilia 16% ya watoto wenye umri mdogo wanauzwa kwa Euro arobaini
elfu kwa kila mtoto, matendo ya aibu kabisa.
Wajumbe wa semina hii wameiomba
Jumuiya ya Ulaya kuhakikisha kwamba, inakusanya takwimu kwa uhakika ili kupambana
kikamilifu dhidi ya biashara haramu ya binadamu pamoja na kuendelea kuwasaidia waathirika
wa mchezo huu mchafu. Hili kundi ambalo linapaswa kulindwa na kuthaminiwa, lakini
wakati mwingine wahanga wa biashara haramu ya binadamu wamekuwa wakiadhibiwa wanapopatikana
na makosa kama haya. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ishirikiane kwa karibu zaidi na vyama
vya kiraia, asasi pamoja na Kanisa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu.