2014-12-02 07:45:43

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa, Rehema kamili kutolewa kwa waamini!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, unaowachangamotisha watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuyapyaisha tena maisha na utume wao ndani ya Kanisa, kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa karama za waanzilishi wa Mashirika yao pamoja na kutoa fursa kwa Familia yote ya Mungu kuweza kufurahia maadhimisho haya katika imani, matumaini na mapendo huku wakiungana na Kanisa zima, Baba Mtakatifu Francisko ametoa zawadi ya rehema kamili kwa waamini wote watakaotimiza masharti yaliyowekwa. RealAudioMP3

Ili kupata rehema kamili, mwamini atapaswa kupokea Sakramenti ya Upatanisho, Ekaristi Takatifu na kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Zawadi hii inatolewa kwa waamini wote watakaotekeleza masharti haya tangu Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, hadi tarehe 2 Februari 2016, Kanisa litakapokuwa linafunga rasmi Mwaka wa Watawa Duniani.

Rehema kamili itatolewa pia kwa waamini watakaosali kwa ajili ya kuombea roho za waamini marehemu, kila wakati watakapokuwa wanashiriki katika matukio mbali mbali ya kimataifa yatakayofanyika mjini Roma kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani; kwa kusali sala ya Baba Yetu, Kukiri Kanuni ya Imani pamoja na kusali Sala zilizokubaliwa na Kanisa kwa Bikira Maria.

Rehema kamili pia itatolewa kwa wale wote watakaotembelea kwenye Makanisa mahalia, nyumba za kitawa au madhabahu maalum yaliyotengwa wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani na kusali Sala ya Kanisa hadharani au ibada nyingine na kuhitimisha kwa kusali Sala ya Baba Yetu, Kukiri Kanuni ya Imani na kumwomba Bikira Maria.

Rehema kamili itatolewa pia kwa watawa ambao kutokana na ugonjwa au sababu mbali mbali watashindwa kuhudhuria katika maeneo yaliyotengwa, kwa kujitenga na dhambi na kunuia kutekeleza mapema iwezekanvyo masharti yaliyotajwa, kwa kufanya hija ya kiroho huku wakitolea mateso na mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa njia ya Bikira Maria na kusali kama inavyotakiwa.

Huu ni mwaliko kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, wanatoa nafasi kwa waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Mpako Mtakatifu kwa ajili ya wagonjwa. Waamini wataweza kupata rehema kamili wakati wote wa Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.