2014-12-02 07:53:51

Kanisa linapania kutangaza Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa!


Askofu mkuu Joseph Edward Kurtz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani anasema kwamba, maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia yalisimikwa katika mambo makuu mawili, mang’amuzi na uamuzi wa pamoja na kwamba, Mababa wa Sinodi walijitahidi kujadili mambo yote katika ukweli na uwazi, ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kutangaza Injili ya Familia. RealAudioMP3

Askofu mkuu Kurtz akizungumzia kuhusu ushiriki wa vyombo vya habari anasema, hii ni Sinodi iliyolenga kuwasaidia Mababa wa Sinodi kusikiliza kwa makini kuhusu changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa kuhusiana na Familia. Hati ya Mababa wa Sinodi inaonesha mwanzo wa safari kubwa ambayo inawasubiri Mababa wa Kanisa, changamoto kwa Familia ya Mungu kuanza kuifanyia kazi kwa ajili ya maadhimisho ya kawaida ya Sinodi ya Maaskofu kuanzia tarehe 4 Oktoba 2015 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.

Askofu mkuu Kurtz anasema, Mababa wa Sinodi katika majadiliano yao, hawakuonesha nia ya kutaka kupingana na Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia, bali kusoma alama za nyakati, ili kuweza kuzisaidia familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Anasema, Hati elekezi ambayo ilikuwa ni mkusanyiko wa mchango wa Mababa wa Sinodi, ilionesha vipengele ambavyo vilitibua nyongo za baadhi ya waamini sehemu mbali mbali duniani, lakini wengi walisahau kwamba, haya yalikuwa ni mawazo tu na wala hakuna maamuzi ambayo yalikuwa yamefikiwa.

Kwa maneno mengine, vyombo vya habari vilitaka kupotosha ukweli kwa kuonesha kwamba, Kanisa Katoliki linakumbatia ushoga. Hati ya Mwisho iliyotolewa na Mababa wa Sinodi baada ya marekebisho ya kina imeonesha msimamo wa Kanisa unaojikita katika Mafundisho Tanzu na Maandiko Matakatifu.

Askofu mkuu Kurtz anamsifu na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuongoza maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, kwa kushiriki kikamilifu wakati wote wa maadhimisho; kwa kusali na kusikiliza kwa makini. Alifungua Sinodi kwa kuwataka wajumbe kuonesha ujasiri, ukweli na uwazi kadiri watakavyojaliwa na Roho Mtakatifu na kwamba hata baada ya maadhimisho ya Sinodi, ujumbe wake umeonesha jinsi alivyokuwa kiungo muhimu katika kuweka mambo sawa!

Kukaa bega kwa bega na Baba Mtakatifu kwa muda wa majuma mawili, kilikuwa kweli ni kipindi cha neema na baraka kwa Familia ya Mungu; ameonesha ari na moyo wa huruma na mapendo kwa familia zinazoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.