2014-12-02 09:41:02

Kanisa lina utambulisho wake na wala si asasi!


Kanisa Katoliki nchini Uswiss linapaswa kuwa ni Sakramenti wazi ya Fumbo la Mwili wa Kristo, kwa kujikita katika kukuza na kudumisha misingi ya amani na utulivu kati ya watu. Uswiss ni makao makuu ya Mashirika ya Kimataifa yanayojihusisha katika mchakato wa kudumisha amani, kazi, sayansi na majadiliano ya kiekumene na kwamba, ushuhuda wa imani una mvuto na mashiko kwa wananchi wengi wa Uswiss.

Waamini wanachangamotishwa kushuhudia imani yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Uwepo wa Makanisa mazuri nchini Uswiss, kama vile Kanisa la Abbasia ya Mtakatifu Moris, linalojiandaa kuadhimisha Jubilee ya miaka 1500 tangu lilipoanzishwa ni kielelezo tosha kabisa cha uhai wa Kanisa, vinginevyo, Makanisa haya baada ya muda si mrefu yatageuzwa kuwa ni majumba ya makumbusho!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe Mosi, Desemba 2014 alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss ambalo linafanya hija ya kitume mjini Vatican. Maaskofu wameambiwa kwamba, utume wao wa kwanza ni kuichunga Familia ya Mungu, kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kushirikiana na Mapadre wao ambao ni wasaidizi wao wa karibu katika dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu nchini Uswiss.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanamwilisha Injili katika uhalisia wa maisha ya wananchi, kama njia ya kujibu kilio cha watu katika medani mbali mbali za maisha. Maaskofu wawamegee waamini wao uzuri na utamu wa Injili, kwa wote wanaoteseka na kutafuta maana mpya katika maisha yao au waamini waliokengeuka na kumezwa na malimwengu. Hili ni kundi ambalo halioni tena umuhimu wa Mungu katika maisha yao; utu na heshima ya binadamu vimewekwa rehani, hasa pale mwanadamu anapopambana na Fumbo la Mateso na Kifo.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo kuonesha ushuhuda wa maisha na imani tendaji inayong'ara, ili kutoa mwanga kwa wale wote wanaotafuta furaha ya kweli katika maisha. Kwa njia hii, Kanisa linaweza kujipambanua katika maisha na utume wake na wala si kama kielelezo cha Asasi kama zilivyo asasi nyinginezo. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kutangaza Habari Njema ya Wokovu na wala wasikubali kumezwa na malimwengu, kwa kutoa majibu muafaka kwa wasikilizaji wao, kwa kuwa na mwono wa kitume, ili kweli watu watambue kuwa, Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu ambaye aliteswa, akafa na kufufuka na wao ni mashahidi wa tukio hili.







All the contents on this site are copyrighted ©.