2014-12-02 10:25:13

Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia nchini Tanzania


TGNP Mtandao ni asasi ya kiraia isiyokuwa na mrengo wa kidini wala kisiasa, iliyoanzishwa na kusajiliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita ikijihusisha na mapambano ya kuleta usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na makundi mengine yalioko pembezoni kwa njia ya ushawishi na utetezi, machapisho na mafunzo kwa njia mbalimbali kupinga ukatili wa kijinsia na kuleta mabadiliko ya kijamii kama sehemu ya haki za binadamu.

Pia TGNP Mtandao hushirikiana na asasi na mashirika mengine ya ndani na nje ya nchi kila mwaka katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Licha ya juhudi mbalimbali za kupambana na ukatili wa kijinsia nchini, bado hali ni mbaya,ambapo takwimu za wizara ya afya zinaonesha, katika mwaka 2013 asilimia 23% ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 19 walikuwa na mimba au walikuwa na watoto huku zikionesha kuwa asilimia 18% ya wasichana wa umri huo huolewa utotoni. Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa bado ukeketaji ni tatizo kubwa likiwa bado linatendeka kwa asilimia 15%.

Kauli mbiu ya kitaifa mwaka 2014 katika kuadhimisha siku hizo ni “Funguka! Fichua Ukatili kwa maendeleo ya jamii”. Katika kuadhimisha siku hizo, TGNP Mtandao itafanya mjadala wa wazi utakaoshirikisha zaidi ya watu 500 kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wanachi kutoka vituo vya TGNP Mtandao vya taarifa na maarifa kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania, makundi yalioko pembezoni, mashirika ya kiraia, wadau wa maendeleo, wasanii na viongozi wa taasisi mbalimbali za umma.

Aidha kauli mbiu ambayo imeongoza mjadala huo ni “Siyumbishwi, Najilinda, Mnilinde” unaojikita kwa vijana hasa wa kike ikiwahimiza wasiyumbishwe, wajiepushe au wajilinde na mambo au mazingira hatarishi na kuitaka jamii iwajibike kuwalinda na kuwakinga vijana dhidi ya ukatili wa kijinsia unaotokea katika mazingira mbalimbali nchini Tanzania.

All the contents on this site are copyrighted ©.