Baraza la Maaskofu Katoliki Uturuki linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kufanya
hija ya kiekumene nchini mwao, kwa kupata fursa ya kukutana, kuzungumza na kusali
pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na kuitia shime Familia ya Mungu nchini
Uturuki, hata katika uchache wao. Hija hii imekuwa ni kikolezo cha ujasiri unaojikita
katika matumaini, ili kuweza kukabiliana na changamoto za ushuhuda wa maisha ya Kikristo
nchini Uturuki.
Baraza la Maaskofu Katoliki Uturuki, linamshukuru Baba Mtakatifu
kwa kuwaonesha njia ya majadiliano ya kiekumene na kidini na waamini mbali mbali wanaoishi
nchini Uturuki. Wakatoliki wanapenda kuendeleza mwaliko uliotolewa na Baba Mtakatifu
unaowataka kufahamiana, kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana katika hija ya maisha
yao hapa duniani; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo yale yanayowaunganisha
zaidi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Uturuki linamshukuru Baba Mtakatifu kwa
kuonesha ukweli kwamba, amani ya kweli inajikita katika kuheshimu haki msingi, utu
na heshima ya binadamu. Familia ya Mungu nchini Uturuki, inapenda kuwa ni mdau mkuu
katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni, kwa kutoa msukumo
wa pekee katika mshikamano wa upendo kati ya wananchi wa Uturuki, ili kujenga na kudumisha
amani na utulivu kati ya watu. Familia ya Mungu nchini humo inapenda kumhakikishia
Baba Mtakatifu Francisko kwamba, itaendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake
kwa njia ya sala na bado wanamwomba aendelee kuiombea Uturuki na watu wake.