2014-12-01 12:19:55

Umoja wa Mataifa unapania kufuta kabisa ugonjwa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030


Bwana Ban Ki-Moon Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2014 anapongeza juhudi ambazo zimekwishafikiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na kwamba, lengo kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, ugonjwa wa Ukimwi unafutika duniani ifikapo mwaka 2030.

Wagonjwa millioni 14 kwa sasa wanapata dawa za kurefusha maisha na kwamba, kuanzia mwaka 2001 iidadi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa UKIMWI imepungua kwa asilimia 38%. Watoto wachanga millioni 1.16 wamekwingwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto. Kufikia Mwaka 2015, wagonjwa millioni 11 watafanikiwa kupata dawa za kurefusha maisha. Hizi ni juhudi zinazofanywa na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI duniani.

Naye Bwana Guy Ryder, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kazi Duniani, ILO katika maadhimisho haya anasema kwamba, waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi ni kati ya kundi kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira duniani. Jumuiya ya Kimataifa itafanikiwa kuondoa ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2030 ikiwa kama, waathirika wa Ukimwi watapewa fursa ya kufanya kazi, huku utu na heshima yao vikipewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kulindwa na jamii husika.

Unyanyapaa, dhuluma na nyanyaso kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi ni kati ya vikwazo vikuu katika mchakato wa upatikanaji wa huduma dhidi ya UKIMWI. Zaidi ya watu millioni 19 hawatambui kwamba, wameambukizwa Virusi vya UKIMWI. Hii inatokana na ukweli kwamba, wafanyakazi wanaogopa kupoteza fursa za ajira ikiwa kama watagundulika kuwa na Virusi vya UKIMWI. Watu wanapaswa kupima kwa hiyari ili kutambua afya zao ili waweze kuwajibika barabara!







All the contents on this site are copyrighted ©.