2014-12-01 07:42:49

Tumieni vyema vyombo vya habari kukuza na kujenga familia!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu pendevu sana cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Leo tunaendelea na udonozi wa hati za Mtanguso Mkuu wa II wa Vatican, tukiwa na lengo la kuuleta ujumbe wake kwa uchache katika familia zetu, ili sisi wanafamilia tukuzwe kwa mafundisho haya ya Mama Kanisa mwenye kutufundisha na kutuelekea katika njia za kweli zinazotupeleka katika mwisho ulio mwema. Kinachotakiwa kwa kila mmoja wetu ni masikio hai ya mwili na roho. Sikia sauti ya Mama na umsikilize ili uokolewe. RealAudioMP3

Leo tunaitazama hati mmoja iitwayo kwa lugha ya Kilatini Inter Mirifica, ikimaanisha ‘kati ya mambo ya kushangaza’! Ni Waraka unaozungumzia umuhimu wa vyombo vya habari katika maisha na utume wa Kanisa. Inter Mirifica ni jina linayopewa hati hii yenye kuzungumzia juu ya vyombo vya upashanaji habari. Kanisa linavitazama na linavipokea vyombo vya upashanaji habari kwa shukrani kwa Mungu aliyempa binadamu akili ya usanifu na uvumbuzi wa kubuni njia hizo zinazoweza kupeleka mawasiliano kwa kasi na hivyo kusaidia pia kazi ya uenezaji wa habari njema ya wokovu kwa watu wote.

Vikitazamwa kwa umakini na kutumiwa kwa uadilifu, vyombo vya upashanaji habari kama vile luninga, magazeti, radio, vitabu, mintandao na simu za aina zote, vinasaidia sana kuiweka jamii ya mwanadamu pamoja. Ni kwa njia ya vyombo hivyo familia ya mwanadamu inawasiliana upesi zaidi na kujisikia imeunganishwa zaidi. Ni vyombo vinavyosaidia kwa upande fulani kuondoa ukiwa na hali ya kujisikia kutengwa au kusahauliwa. Vinatusaidia kujipatia taarifa na maarifa juu ya maisha halisia ya kila siku.

Lakini kwa upande mwingine binadamu kwa ubaya wa moyo wake anaweza pia kutumia vyombo hivyo kwa uharibifu wake na wa wengine wengi, hasa watoto na vijana wasio na mwelekeo thabiti. Kwa njia ya hati hii, Kanisa lilidhamiria kuelekeza ili vyombo hivyo vyote vitumike vema kwa kueneza habari njema, maadili na taarifa za kweli ili watu wakabili maisha vizuri na mwishowe wapate kuokoka.

Kichungaji, sisi waamini tunaalikwa kwa hali na mali kuchangia sana katika kudumisha sekta ya upashanaji habari katika Kanisa. Redio, tovuti na luninga zetu ni za msaada mkubwa sana katika uinjilishaji kwa nyakati zetu hizi. Leo tunashukuru kabisa msaada wa vyombo vya mawasiliano, mambo mengi mazuri yanatufikia, na yanakwenda hadi pembezoni kabisa mwa dunia.Tuone kuwa ni wajibu wetu sote kuchangia uendeshaji wa vyombo hivi ili Injili ya Kristo iende mbele zaidi na zaidi.

Katika sehemu zile ambapo kuna Radio za Kanisa, waamini tuamke hasa tuchangie ufanisi wa vyombo vile. Vyombo hivyo vinapeleka sauti ya wokovu pale ambapo wewe mwenyewe ulipaswa kwenda lakini umeshindwa. Basi uende huko kwa njia ya mchango wako. Mwito pia kwa Wakristo wanaomiliki vyombo vya habari, kujitahidi kusambaza mafundisho adilifu, kusambaza ujumbe wa amani na kuliko kuchangia umomoaji wa maadili, kusambaza chuki na kuchochea vurugu.

Na inapowezekana vyombo vya mawasiliano vya Wakristo visambaze pia cheche za neno la Mungu, ili kuchangia katika kujenga dhamiri za watu na jamii adilifu, kusaidia kuuimarisha ufalme wa Mungu mioyoni mwa watu. Vijana katika simu zetu tusambaze jumbe adilifu, tupasiane neno la Mungu. Wale mabingwa wa kutengeneza tovuti, tutengeneze hata tovuti za uinjillishaji kwa makundi mbalimbali. Vyama vya kitume pia vinaweza kuwa na tovuti zao maalumu za uinjilishaji. Nyakati hizi za uinjilishaji mpya na wa kina, tutumie pia vyombo hivi vya mawasiliano ili kumpata binadamu wa sasa hukohuko aliko. Wamisionari ni mimi na wewe. Tutimize wajibu huu kwa ubunifu na uadilifu, ili Mungu atukuzwe na sisi tuokolewe. Tukitaka, tunaweza na tutaweza.

Katika hati hii Kanisa lililenga pia kuwaelimisha watu wote wote kuhusu namna ya kuchuja na kutumia vyombo hivyo kwa busara, pasipo kudumbukia katika mtengo wa kukusanya kichwani kila aina ya habari na kuiamini na kuiweka katika maisha. Kanisa halikukwepa ukweli kwamba, vipo vyombo ambayo hupotosha ukweli husambaza sumu mbaya ya chuki na vurugu; na mwishowe husababisha kuenea kwa uovu na uhaini mkubwa kwa familia ya mwanadamu.

Ni mwito kwa wazazi na hata serikali kujaribu kuratibu vema mambo yale yanayoingia katika mitaala ya elimu kwa njia ya mitandao, yasiwe chanzo cha kujenga akili-tundu na angamizi kwa watoto wetu. Kwa kila mmoja wetu kinachoalikwa zaidi ni matumizi adilifu ya vyombo vya mawasiliano. Historia zitashuhudia kwamba, nyakati zetu hizi, utamaduni wa kusema uwongo umekua kwa kasi sana, wizi wa kimitandao unakuwa na kuchukua sura mpya kila kukicha. Watu binafsi na taasisi mbalimbali zimekwishaingia katika hasara kubwa kwa sababu ya kuibiwa kimitandao.

Ufitanishi kwa njia za simu za mkononi umekua sana, ufitanishi ambao tayari umeziweka ndoa nyingi makorongoni. Watu wengi wameingiliwa katika faragha zao na wameaibishwa vibaya, sura zao katika jamii zimebomolewa kwa sababu ya watu kukosa uadilifu katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano. Vyombo vyetu hivyo badala ya kujenga utu, vinararua na kubomoa kabisa utu wa mtu. Leo hii upende usipende utapigwa picha mahali popote tu na picha itaanikwa katika mitandao. Watu hawaoni aibu tena kuwaangamiza wenzao kwa njia ya mitandao. Hatuwezi kukwepa uhalisia huo, tujilinde tu. Yoshua Bin Sira anafundisha akisema, ‘ mwanangu, uwe mwangalifu kwani unatembea katika hatari’.

Tunapotafakari juu ya umuhimu wa mawasiliano na vyombo vya upashanaji habari, tunapenda kualikana, kila mmoja wetu awe ni mjumbe wa habari njema, mjumbe wa amani. Tuweke kando vyombo tulivyoviainisha hapo juu. Turudi katika uhalisia wetu wa kawaida; sisi wanadamu tunavyo vyombo vyetu asilia vya mawasiliano, ambavyo ni midomo yetu, miguu yetu, macho yetu na masikio yetu, navyo hivyo vyote huongozwa na akili zetu zenye kujenga mawazo. Tunapenda kukumbushana tu juu ya matumizi adilifu ya midomo yetu. Vinywa vyetu vitangaze sifa ya Bwana. Miguu yetu iwe ni ya mtu apelekaye amani kwa watu.

Mwisho tunatoa rai ya pekee sana kwa Kanisa la nyumbani; vyombo vya mawasiliano, visitunyang’anye utu wetu na kujenga visiwa ndani ya familia. Siku hizi katika familia nyingi, watu wanaishi pamoja wanapishana milangoni, lakini wanashindwa kuketi na kuzungumza na kusikilizana katika mambo ya msingi kabisa ya kifamilia au ya mahusiano yao. Baba na mama watawasiliana kwa njia ya ujumbe wa simu au barua pepe tu. Watatukanana bila aibu, watashutumiana, watanyanyasana kwa njia ya mitandao.

Na siku nyingine, habari tete za ndoa mwanandoa badala ya kuongea na mwenzake, anazianika tu kwenye mitandao, ili tu kumkomesha mwenzake. Muda woote, mzee yupo na TV au radio anacheeka sana, na mama naye yuko bize na simu saba mkononi zenye mitandao yote ya kijamii, amejaa tabasamu lote. Lakini wao wenyewe huwezi kuwakuta wanatazamano usoni wala kuchekeana. Polepole ukuta mkubwa sana unajengwa kati ya wanandoa hawa. Utu wao wammeukodisha kwa mitandao! Hapo lazima mchwa ataingia tu katika familia hiyo.

Na wakati mwingine wazazi hawana muda wa kuona sura za watoto wao na kuzungumza nao, wanawasiliana tu kwa njia ya mitandao. Matokeo yake kuna kuna hali ya ugeni wa ajabu unajengeka katika familia. Mitandao ni mizuri lakini tuangalie isitusahaulishe kwamba sisi ni viumbe-jamii tunaohitaji mawasiliano ya ana kwa ana. Tukianza kudharauliana na kusahauliana sisi tulio sura na mfano wa Mungu, je tutaweza kweli kumkumbuka Muumba mwenyewe?

Kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.