Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis
katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa
kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Desemba linasema kwamba, kila mtu anapaswa kupata
maisha bora na kuhudumiwa kwa heshima ya tahadhima, changamoto iliyotolewa hivi karibuni
na Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema!
Lengo
hili linaweza kufikiwa ikiwa kama jamii itafanikiwa kuvunjilia mbali kuta za utengano
kwa kuwakumbatia wote wenye shida na mahangaiko yao ndani; kwa kuheshimu na kuthamini
utu wao kama binadamu pamoja na kuwahudumia kwa moyo wa upendo na huruma.
Takwimu
zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya millioni 39 waliofariki kutokana na ugonjwa
wa Ukimwi pamoja na magonjwa mengine nyemelezi katika kipindi cha miaka thelathini
iliyopita. Caritas Internationalis, wakati wote huu, imetembea na waathirika wa ugonjwa
wa Ukimwi kwa kuwajengea uwezo, ili kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha,
changamoto ya kuendelea kuboresha huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi pamoja
na kupunguza maambukizi mapya; kwa kuonesha mshikamano pamoja na kutafuta mafao ya
wengi pamoja na kutoa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wapatao millioni 25; kwa
kuendelea kuzuia maambukizi mapya; kwa kuwaonesha upendo wagonjwa na waathirika wa
Ukimwi pamoja na kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi ambao wakati mwingine inakuwa
ni vigumu kwao kupata huduma za afya.
Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili
ya watoto, kwa kuwapatia huduma zitakazozuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto wakati wa kujifungua pamoja na kupambana na umaskini, ili watu wengi waweze
kupata dawa za kurefusha maisha, huku utu wao ukiheshimiwa na kuthaminiwa,kwa kuongozwa
na kanuni ya upendo kwa Mungu na jirani.