2014-12-01 08:32:36

Papa arejea mjini Vatican baada ya hija yake ya kiekumene nchini Uturuki


Mara baada ya kuhitimisha hija yake ya kiekumene nchini Uturuki, iliyomwezesha kukutana na kusali na waamini wa dini mbali mbali nchini Uturuki, ili kujenga udugu na umoja, haki na amani miongoni mwa jamii, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili alasiri tarehe 30 Novemba 2014 alifunga vilago na kurejea tena mjini Vatican. Lakini kabla ya kuondoka kurejea Vatican, Baba Mtakatifu alimtembelea na kumsalimia Patriaki Mesrob Mutafian wa Kanisa la Kiarmeni la Costantinopol, ambaye ni mgonjwa sana na amelazwa kwenye Hospitali ya San Salvatore mjini Istanbul, Uturuki.

Akiwa njiani, amewatumia ujumbe wa matashi mema Marais wa Ugiriki, Albania na Italia. Akiwa kwenye hanga za Ugiriki, Baba Mtakatifu amemtakia Rais Karolos Papoulias baraka za mshikamano na amani kwa wananchi wa Ugiriki. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Rais Bujar Nishani wa Albania, amewatakia amani, neema na baraka anaporejea kutoka katika hija yake ya kiekumene nchini Uturuki.

Baba Mtakatifu amemwambia Rais Giorgio Napolitano wa Italia kwamba, akiwa nchini Uturuki, amebahatika kukutana na kuzungumza na makundi mbali mbali ya wananchi wa Uturuki na amewaonesha moyo wake wa shukrani, hasa kutokana na utajiri mkubwa unaofumbatwa katika historia na maisha ya wananchi wa Uturuki. Amewasihi kuendeleza mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani, kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene. Anawatakia wananchi wote wa Italia umoja na mshikamano wa kweli.

Akiwa angani, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu hija yake ya kiekumene pamoja na kujibwa maswali kadhaa, mazungumzo ambayo yamedumu kwa takribani masaa matatu na robo!

Baba Mtakatifu Francisko alipowasili jioni kwenye Uwanja wa ndege wa Ciampino amepokelewa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Italia na baadaye akaelekea moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, kummshukuru Bikira Maria aliyemsimamia na kumwongoza katika hija yake ya kiekumene nchini Uturuki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.